Dar es Salaam. Tukio la watoto kudaiwa kumzika baba yao mzazi akiwa hai, limezidi kuchukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kuwatia mbaroni watu 12. Watoto hao walimzika hai baba yao Florence Komba (78) kwa kumtuhumu mshirikina na kuhusika kwenye mauaji ya mwanaye Severeni Komba (34).
Komba aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Mahanje katika Halmashauri ya Madaba, alizikwa akiwa hai Agosti 12, mwaka huu akituhumiwa kumuua Severine kishirikina.
Mzee huyo inadaiwa alifariki dunia baada ya watoto wake wawili kushirikiana na vijana wa kijijini hapo kumzika kwenye kaburi lililoandaliwa kwa ajili ya maziko ya Severine aliyefariki akiwa ndani kwake baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Pili Mande alisema alithibitisha kuwashikilia watuhumiwa hao 12 wakiwamo watoto wawili wa marehemu huyo.
“Mpaka sasa (juzi) tunawashikilia watu 12 wakiwamo watoto wawili wa mzee Komba. Watuhumiwa hawa wakati wakijiandaa kwenda kumzika Severine, walitangulia kutoka kanisani wakitumia guta na walipofika makaburini kabla ya watu wengine kufika, waliweka jeneza la marehemu pembeni na kumuingiza baba yao kwenye kaburi na wakamzika,” alisema Kamanda Pili.
Alisema vijana hao walifanya kitendo hicho kwa kumtuhumu baba yao kuwa ndiye aliyehusika na kifo cha mdogo wao kwa kumroga kichawi.
“Huyo mdogo wao alikufa kifo cha kawaida na maziko yalifanyika Agosti 12, lakini hao vijana walipofika kaburini walimlazimisha baba yao kuwa wanaanza kumzika yeye kwa kuwa ndiye amesababisha kifo cha mdogo wao,” alisema.
Akisimulia jinsi Mzee Komba alivyochukuliwa na kupelekwa makaburini, Kamanda Pili alisema siku ya tukio, vijana hao walikodi pikipiki ya magurudumu matatu maarufu kama guta kwa ajili ya kubebea jeneza la Severine na kumtaka baba yao naye apande ili watangulie naye makaburini.
Baada ya kufika makaburini kabla ya watu wengine kufika, alisema vijana hao walimlazimisha mzee huyo aingie kaburini na wakamzika huku jitihada zake za kujiokoa zikigonga mwamba hivyo, kuhitimisha maisha yake hapa duniani.
“Walimzika akiwa hai, baadaye watu walipofika wakakuta jeneza liko pembeni na kaburi limefukiwa. Walitoa taarifa polisi lakini wengine wakaanza kulifukua ila wakakuta tayari Mzee Komba amefariki,” aliongeza Kamanda Pili.
Hata hivyo, Kamanda Pili alisema licha ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao 12 bado Polisi linaendelea na uchunguzi kuwabaini wote waliohusika katika tukio hilo.
Alisema muda wowote watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji zinazowakabili.