Uongozi wa Klabu ya Yanga na Kamati ya Utendaji chini ya Rais Eng.Hersi Said umesema umepokea kwa masikitiko taarifa ya ajali ya Mashabiki wa Yanga waliokuwa wakielekea Arusha kuishangailia Timu yao kwenye Mchezo wa Ligi Kuu.
Yanga imesema ajali hiyo imepelekea kifo cha Shabiki maarufu wa Yanga Almaarufu Dada Hadija ambapo Uongozi wa Yanga umetoa pole kwa Wasafiri wote na Familia ya Dada Hadija na kutoa shukrani kwa wote walioshiriki katika kuokoa majeruhi kwenye ajali hiyo.
Itakumbukwa jana usiku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo aliithibitishia @ayoTV_ na millardayo.com kuwa Watu watano walijeruhiwa usiku baada ya gari (Coaster) lililobeba Mashabiki wa Yanga waliokuwa wanatokea Dar es salaam kuelekea Arusha kupata ajali baada ya kugongwa ubavuni na Canter iliyokuwa imebeba mihogo katika eneo la Kiwangwa Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Lutumo alisema chanzo cha ajali ni gari lililobeba Mashabiki wa Yanga kutaka kuover-take na Dereva wa Canter akapambana kukwepa kukutana uso kwa uso na Coaster hiyo na kuishia kuigonga ubavuni na ikapata ajali ambapo Majeruhi walikuwa watano na wawili ndio walikuwa mahututi akiwemo Dada Hadija ambaye ameripotiwa kufariki.