SIMBA na Yanga zinatumia wachezaji wenye viwango vya juu, hivyo kunakuwa na ushindani wa kuwania namba kwa mastaa hao ili kuwashawishi makocha kuwapanga vikosi vya kwanza.
Ndivyo pia ilivyokuwa msimu ulioisha kwani wapo waliotegemewa vikosi vya kwanza na wengine wakajikuta wanasugua benchi.
Tayari msimu mpya umeanza na zimechezwa raundi mbili, hivyo kuna fursa kila mchezaji kushtuka mapema na kuanza kupambania namba, hasa wale ambao hawakuwa na nafasi msimu ulioisha.
Mwanaspoti linakuchambulia mas taa ambao watatakiwa kuupiga mwingi ili makocha wawaamini kwenye vikosi vyao vya kwanza.
ERICK JOHORA - YANGA
Ukiachana na ubora wa kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra, Johora atatakiwa kupambania namba na kipa namba mbili, Aboutwalib Mshery ambaye akipewa nafasi anaonyesha kiwango cha juu, kilichofanya ajumuishwe kwenye kikosi cha Stars.
CRISPIN NGUSHI -YANGA
Kutokana na nafasi yake kuwepo mastaa wanaojua kutupia na wamekuwa kwenye kiwango cha juu kama Fiston Mayele ambaye msimu ulioisha alimaliza mfungaji wa pili na mabao 16 ya Ligi Kuu Bara, Ngushi anatakiwa kukaza buti ili kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza.
SHAIBU ‘NINJA’ - YANGA
Katika nafasi beki wa kati wanacheza Bakari Mwamnyeto na Dickson Job wanaoitwa kwenye kikosi cha Stars, jambo ambalo linampa kibarua kigumu beki wa kati Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kupambania nafasi kikosi cha kwanza. Mchezaji mwingine ambaye ana kazi ya kumshawishi kocha Nsreddine Nabi katika nafasi hiyo ni Ibrahim Abdallah ‘Bacca’.
HERITIER MAKAMBO - YANGA
Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi bado ana imani na Makambo anayepitia wakati mgumu wa ukame wa mabao, akimpa nafasi ya kucheza msimu huu alimuanzisha kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa pili wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union, kisha akamtoa na nafasi yake ikachukuliwa na Fiston Mayele ambaye alifunga bao la pili kwenye ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-0. Mwanzo huu wa ligi ni fursa kwa Makambo kupambana kurejea kwenye makali yake.
ZAWADI MAUYA - YANGA
Japokuwa hana uhakika wa kucheza kikosi cha kwanza, Mauya ni kiungo ambaye akijituma kwa bidii na kushtuka mapema anaweza kuwa mchezaji muhimu ndani ya timu. Katika nafasi yake anashindana na kina Gael Bigirimana, Yannick Bangala na Khalid Aucho.
DAVID BRYSON - YANGA
Tangu beki David Bryson asajiliwe na Yanga msimu uliopita akitokea KMC, hajapata nafasi ya kuwa muhimu kikosi cha kwanza. Anacheza kwa nadra na tayari katika nafasi yake kasajiliwa Joyce Lomalisa kutoka Sagrada Esperança ya Angola huku pia muda mwingine akicheza Kibwana Shomari.
ALLY SALIM - SIMBA
Tangu apandishwe timu ya wakubwa, amekuwa hana nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mbele ya kipa namba moja Aishi Manula na namba mbili Beno Kakolanya, hivyo ana kazi kubwa kuhakikisha anapigania nafasi kikosini.
JOHN BOCCO - SIMBA
Msimu ulioisha alimaliza na mabao matatu, hivyo msimu huu anatakiwa ashituke mapema ingawa ana rekodi ya aina yake ya kumiliki mabao mengi - 145 kwa wachezaji wanaocheza sasa. Katika nafasi yake anashindania namba na washambuliaji Habibu Kyondo, Dejan Georgijevic na Kibu Denis.
ERASTO NYONI - SIMBA
Ni mchezaji kiraka ambaye tangu msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara anaonekana kutopewa nafasi kubwa ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza cha Simba. Hata hivyo katika Ligi Kuu inayoendelea kwa sasa anatakiwa kushtuka mapema ili kumshawishi kocha Zoran Maki na benchi lake la ufundi kumpanga mara kwa mara.
Katika nafasi ya beki ambayo pia anaimudu wapo Henock Inonga, Joash Onyango na ingizo jipya Mohamed Quattara huku mchezaji mwingine anayesotea namba ni Kennedy Juma licha ya kwamba pia kaitwa kikosi cha Stars.
VICTOR AKPAN - SIMBA
Tangu asajiliwe na Simba akitokea Coastal Union ya Tanga katika mechi mbili Ligi Kuu hajacheza hata moja. Katika nafasi yake yupo Jonas Mkude, Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute. Ukiachana na hao yupo pia mchezaji mwingine mpya ambaye ni Nassor Kapama anayetakiwa kupambania namba.