Mbowe ahoji utitiri wa magari msafara wa Rais




Dar/Shinganga. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema utitiri wa magari katika msafara wa Rais Samia Suluhu Hassan hauendani na dhana ya Serikali ya kubana matumizi.

Amesema, gharama za maisha zinatesa wananchi huku Serikali ikionekana kutodhihirisha kwa vitendo mkakati wake wa kubana matumizi

Mbowe aliyasema hayo juzi mkoani Shinyanga alipokuwa akihutubia wanachama wa chama hicho katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani iliyoandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Alisema hivi karibuni alimwandikia ujumbe Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Chemba kumweleza kodi na tozo wanazotoza kwa wananchi haziakisi uhalisia na kuchochea umaskini miongoni mwao.


“Kodi hutozwa matajiri ili kuwasaidia maskini, unategemea nini kwa wananchi hawa unapowatoza kipato chao kidogo? Sasa wenzetu hawa hawaelewi, nilimuandikia barua Dk Mwigulu kuhusu hili mpaka sasa sijapata majibu” alisema

Alisema: “Gharama za kuendesha Serikali kila siku zinapanda, Rais anatembea na msafara wa magari karibu 70 hadi 80 Land Cruiser za kazi gani? Hivi kweli nchi hii na umaskini wake unatumia magari yote haya, waziri mkuu, makamu wa Rais.”

Mbowe alitolea mfano Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na Naibu wake wawili, Salum Mwalimu (Z’bar) na Benson Kigaila (Bara) wote watatu wametumia gari moja kutoka Dar es Salaam hadi Shinyanga ili kubana matumizi.


Kiongozi huyo wa upinzani ametoa kauli hiyo wakati Rais Samia akiendelea na ziara za kikazi mkoani Iringa akitokea Mkoa wa Njombe na Mbeya alikoanzia.

Lengo la ziara hiyo iliyoanza Agosti 5 mwaka huu ni kukagua, kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

Mbowe alitumia kongamano hilo pia kuelezea mazungumzo baina ya Chadema na CCM yanayoendelea akisema: “tunayachukulia mazungumzo haya kwa tahadhari kubwa sana.”

Mazungumzo hayo yalianza kwa Mbowe kukutana na Rais Samia Ikulu jijini Dar es Salaam na baadaye timu ya chama hicho ikiongozwa na Mbowe na ile ya Serikali ikiongozwa na Rais Samia zilikutana jijini Dodoma.


Mbowe alisema baadhi ya mambo waliyokubaliana ni kufutwa kwa kesi za kisiasa, kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa, Katiba Mpya na hakikisho la usalama kwa wakimbizi wa kisiasa.

Mbowe alisema nyadhifa za waliokuwa wabunge wao Halima Mdee na wenzake 18, waliokuwa wanachama wa Chadema ndiyo jambo pekee waliloshindwa kufikia muafaka na limeachwa mikononi mwa Mahakama.

“Wamekwenda mahakamani kutetea wasivuliwe ubunge wao, kwa sababu hayo yapo mahakamani hayawezekani kuzungumzwa kwenye kamati, hivyo tumeiachia Mahakama ifanye kazi yake huko itajulikana mbivu na mbichi” alisema Mbowe

“Baada ya mazungumzo tulikubaliana kuunda timu ndogo ambazo zitahusika katika kuchambua hoja moja baada ya nyingine kati ya 20 tulizoziwasilishwa ili kuona tutakapofikia,” alisema.


Katika kufanikisha hilo, alisema timu za watu watano kila upande ziliundwa Chadema ikiongozwa na Mbowe na CCM ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Abdulrahman Kinana.

Kwa mujibu wa Mbowe, timu hizo ziliamua kutafuta muafaka wa hoja tano za mwanzo ikiwemo Katiba Mpya na watakutana tena Agosti 17 na 18 mwaka huu, kisha baadaye watajadili kuhusu vifungu na hatua nyingine.

Aliitaja ajenda nyingine ni Serikali kukimbiza au kufuta kesi na kusamehe wafungwa wote wa kisiasa na kufafanua kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 zaidi ya wanachama na viongozi 200 wa chama hicho walifungwa na wengine kushtakiwa. “Tunapozungumza sasa zimebaki kesi nne na watu saba ndiyo wapo magereza, tumekubaliana Rais aone umuhimu wa kuwatoa kwa msamaha na kuacha kuzalisha wafungwa wapya wa kisiasa,” alisema.

Alisema suala lingine ni kurejeshwa kwa haki za kufanya siasa na mikutano ya hadhara akifafanua kuwa hilo limebaki kuwa suala la kisheria.

Alisema jambo lingine walilojadili ni kutolewa kwa hakikisho la usalama kwa wakimbizi wa kisiasa, jambo ambalo Rais Samia ameshamwagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni na tayari ameshafanya hivyo bungeni.


Alieleza kukerwa na wanaomshutumu kwamba amelambishwa asali, akisema ataendelea kuwa na misimamo kama aliyokuwa nayo awali.

“Nilichagua kufa nimesimama kuliko nimepiga magoti, nimepoteza mali na biashara zenye thamani kubwa, muda sahihi ukifika nitadai kilichokuwa halali yangu tena bila kificho, kwani Serikali hii imedhulumu kilicho changu hadharani” alisema.

Katika hatua nyingine, mwanasiasa huyo aliwataka vijana kuacha kulalamika, badala yake wawe msingi wa mabadiliko kwa kuiwajibisha Serikali.

Alieleza kusikitishwa na mfumo wa elimu nchini, ambao unazalisha wataalamu wasiokuwa na ushindani katika soko la ajira duniani.

“Kila mtoto anazaliwa na akili lakini anatakiwa kuwa na elimu bora, kuna watoto milioni 1.4 wasiokuwa na ajira tumeruhusuje.

“Maana kila mwaka wanaingizwa mitaani na mwenye wajibu wa kuhakikisha watoto hawa wanapata elimu ni Serikali iliyopo madarakani,” alisema.

Hata hivyo, alisifu uchaguzi Mkuu uliofanyika Kenya, akisema Tanzania ina mambo ya kujifunza katika hilo.

Akizungumzia Katiba Mpya, Katibu Mkuu chama hicho, John Mnyika alisema kinachohitajika iwe na maudhui ya Watanzania wote.

“Katika hili asibaki mtu nyumaWatanzania wote washiriki na maoni yao yapewe nafasi,” alisema Mnyika.

Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad