Mbowe Avunja Ukimya Kuhusu Ikulu



Mwenyekiti wa Chadema Taifa Freeman Mbowe akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya vijana Duniani yaliyofanyika Kitaifa mkoani Shinyanga kwa kuratibiwa na Vijana wa Chadema BAVICHA.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, amezungumzia ukimya wake mara baada ya kutoka Ikulu kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa hakupewa kitu chochote (Asali) kwa ajili ya kunyamazishwa akieleza kuwa amekuwa na ukimya kwa sababu siyo kila muda lazima azungumze hasa katika kipindi hiki ambacho wapo kwenye maridhiano ya kisiasa.

Amebainisha hayo leo Agosti 12, 2022 kwenye Maadhimisho ya siku ya vijana duniani ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Shinyanga, yakiratibiwa na Baraza la vijana wa Chadema (BAVICHA).

Amesema yeye hakurambishwa Asali Ikulu, bali ana misimamo yake na hana tamaa, na angekuwa na njaa siku nyingi angekuwa ameshaipiga bei Chadema na kuhama nchi, lakini yupo kwa ajili ya kupigania maslahi Watanzania kwani yeye ni mpenda haki.

“Ukimya wangu siyo kwamba nilirambishwa Asali Ikulu,na kama ningetaka kurambishwa Asali ningerambishwa siku nyingi tu siku za nyuma tena nilikuwa napewa na vitisho, lakini mimi siyo wa hivyo, nimenyamaza kwa sababu kila jambo na wakati wake,”amesema Mbowe.

“Ningekuwa na Shida, ningekuwa mtu wa hasira, visasi na vinyongo, na wakati mimi napambana kupigania haki za wafungwa na maslahi ya Watanzania, mtu mwingine anakazana mitandaoni eti ukimya wa Mbowe amelishwa Asali Ikulu unamjua Mbowe wewe,”ameongeza.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema Taifa (BAVICHA) John Pambalu, amesema wameadhimisha Siku ya  vijana duniani kitaifa mkoani Shinyanga ili kujadili ajenda mbalimbali kwa mustakabali wa maisha ya vijana ikiwamo na kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Kwa upande wake Katibu Mkuu cha Chadema John Mnyika, amesema Chama hicho kitaendelea kupigania upatikanaji wa Katiba Mpya, ambayo ndiyo itakuwa suluhisho la matatizo yote hapa nchini, kwa kupata viongozi ambao wanatokana na wananchi, na kutatua matatizo yao na siyo kuongozwa na viongozi wa kuchaguliwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad