MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kamwe hawezi kukiuza chama hicho, bali ataendelea na msimamo wake wa kupigania haki za Watanzania.
MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Vilevile amedai alishapokea vitisho vingi na hata kupewa fedha ili akiuze chama hicho na akapoteza mali zake nyingi za mamilioni ya shilingi, lakini hakufanya hivyo na ameendelea kusimama na wanachama wake na kwamba anajipanga kufungua kesi kudai mali zake hizo.
Mbowe alitoa kauli hiyo juzi mkoani Shinyanga alipozungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ambayo yalifanyika mkoani hapa yakiratibiwa na Baraza la Vijana wa Chama hicho (BAVICHA) chini ya Mwenyekiti wake, John Pambalu.
Alisema baada ya kutoka Ikulu kuzungumza na Rais Samia na kuwa mkimya kwa muda, kuna maneno yalianza kuzungumzwa mtandaoni kuwa ukimya wake huo ulikuwa ishara kwamba tayari 'ameshalambishwa asali Ikulu', jambo ambalo alilikanusha vikali, akisisitiza hawezi kufanya hivyo.
“Ukimya wangu mara baada ya kutoka Ikulu kuzungumza na Rais Samia siyo kwamba nililambishwa asali, hapana! Watu wanapaswa kuelewa kwamba nimenyamaza kwa sababu kila jambo na wakati wake, mimi ningekuwa na njaa siku nyingi CHADEMA ningekuwa nimeipiga bei na kuhama nchi.
“Kama kuiuza CHADEMA kwa kulambishwa asali, ningekuwa nimeiuza kipindi cha nyuma ambapo nilikuwa nikipokea vitisho na kupoteza mali zangu za mamilioni, mimi siyo mtu wa njaa na sina tamaa, ninapenda vya halali," Mbowe alisisitiza.
Alisema licha ya kupoteza mali zake hizo wakati akipokea vitisho, muda ukifika atafungua kesi kudai haki zake, akisisitiza 'nikipewa sawa na nikikosa sawa', huku akibainisha kuwa kamwe hawezi kutawaliwa na mali, bali yeye ndiyo anaitawala mali.
Katika mkutano huo, Mbowe pia alizungumza suala la maridhiano ya kisiasa kati ya serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CHADEMA ili kujenga misingi ya uhuru, demokrasia, haki na maendeleo bila ya ubaguzi wa kiitikadi.
Alitaja hoja tano za awali ambazo kwa sasa ndiyo wapo kwenye hayo maridhiano, kuwa suala la upatikanaji wa Katiba Mpya, serikali kufuta kesi zote za kisiasa na kusamehe vifungo kwa madai kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2020 wanachama wa chama hicho wengi walibambikwa kesi, lakini akakiri kwamba kesi nyingi zimefutwa na kubaki nne.
Alitaja hoja ya tatu ni kurejesha mikutano ya hadhara kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kwa sasa wapo katika hatua nzuri.
Hoja nyingine ni kuhusu Halima Mdee na wenzake, lakini akasita kulizungumzia kwa kina suala hilo kwa kuwa liko mahakamani.
Kwa mujibu wa Mbowe, hoja ya tano ni kuwarudisha wakimbizi wa kisiasa ambao walikimbilia nje ya nchi na serikali iwahakikishie ulinzi ili wapate kurejea, jambo ambalo alisema liko katika hatua nzuri na watu hao wanakaribishwa kurejea nyumbani.
Alizungumzia pia hali ya vijana nchini, akisisitiza kuwa kuna mamilioni ya vijana kila siku wanazaliwa, lakini kasi yake haiendani na kasi ya ukuaji wa uchumi nchini, hivyo wengi wao kukabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), John Pambalu, alisema tatizo kubwa ambalo bado linawakabili vijana wengi nchini ni ukosefu wa ajira na mitaji ya kuwawezesha kujiajiri wenyewe.
Alisema licha ya serikali kutangaza fursa za mikopo kwa ajili ya vijana, fedha hizo 'zinapigwa' na watumishi, akiutolea mfano Mkoa wa Mwanza ambazo moja ya halmashauri Sh. bilioni 4.9 zimetafunwa na watumishi.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alisema suluhisho la matatizo yote hayo ni upatikaji wa Katiba Mpya, ambayo ndiyo mkombozi kwa Watanzania pamoja na kupata viongozi sahihi waliowachagua na siyo kuchaguliwa viongozi.