Meya amfukuza diwani kikaoni



Mwanza. Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga amemfukuza Diwani wa Kata ya Kitangiri, Donald Ndaro katika kikao cha baraza la madiwani kinachofanyika katika ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo kwa madai ya utovu wa nidhamu

Baada ya kufukuzwa diwani huyo alisimama kwa dakika zaidi ya tano akisubiri hoja za kumtetea kutoka kwa madiwani wenzake jambo ambalo liligonga mwamba baada ya mwanasheria wa ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Patrick Muhere kupigilia msumari kwamba Kanuni za Halmashauri za Uendeshaji wa Vikao hazimruhusu diwani huyo kuhudhuria kikao hicho.

Akizungumza na Mwananchi Digital katika mahojiano maalumu, Mulunga amesema uamuzi wa kumzuia diwani huyo kuhudhuria katika vikao viwili ulitolewa jana Alhamisi kutokana na utovu wa nidhamu.

Mulunga ameiambia Mwananchi Digital leo Ijumaa Agosti 26, 2022 kwamba diwani huyo (Ndaro) pamoja na kukatazwa kuzungumza bila ruhusa kutoka kwake ambaye ndiye mwenyekiti wa vikao vya baraza hilo alikaidi na kuendelea kuzungumza jambo lililosababisha usumbufu kwa wajumbe wa kikao hicho.


"Nimemfukuza leo kwa sababu alionyesha utovu wa nidhamu kwenye kikao cha baraza kilichofanyika jana (Alhamisi). Lakini nimeshangaa amehudhuria kikao cha leo ndiyo maana nimemfukuza hadi hapo adhabu yake itakapokoma," amesema Mulunga.

Awali, Diwani huyo aliyefukuzwa, Donald Ndaro alipoulizwa na meya huyo kwa nini amehudhuria kwenye kikao hicho wakati ana adhabu ya kutumikia alisema kanuni inamruhusu kuhudhuria kikao hicho.

Hata, hivyo baada ya kufukuzwa alitoka nje ya ukumbi na kuondoka eneo hilo huku juhudi za kumtafuta kwa simu kuzungumzia kufukuzwa kwake zikigonga mwamba baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.

Katika hatua nyingine, baraza hilo limemteua, Diwani wa Kata ya Buzuruga, Manusura Lusigalite kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Lusigalite amechanguliwa katika nafasi hiyo kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya kupigiwa kura za ndiyo na wajumbe 23 wa mkutano huo huku akiwashukuru wajumbe na kuahidi kusimamia fedha za umma kwa weledi.

"Ninawashukuru kwa kuniamini jukumu letu kubwa ni kuhakikisha fedha za wananchi zinasimamiwa na kutumika katika matumizi yaliyopangwa. Pia kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na ubora unaohitajika," amesema Lusigalite.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad