MIILI ya watu watatu imeokotwa ikiwa imefungiwa kwenye mifuko ya sandarusi maarufu viroba, baada ya kutupwa na watu wasiojulikana katika Kitongoji cha Dibabara, Kijiji cha Kwastemba, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi Safia Jongo.
Inaelezwa kuwa, mwili mmoja uliokotwa katika Kata ya Tunguli, baada ya gari moja aina ya Toyota Landcruiser kupita katika eneo la Dibabara, Agosti 11 mwaka huu majira ya saa moja usiku.
Alipotafutwa kuzungumzia taarifa za kuokotwa kwa miili hiyo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi Safia Jongo, alisema anafuatilia matukio hayo na atatoa taarifa kwa vyombo vya habari wakati wowote.
Katika tukio la kwanza, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tunguli, Omary Mtoi, alidai kuwa wakazi wa Kitongoji cha Dibabara, ambao ni jamii ya wafugaji ya Kimasai, waliona gari lenye rangi nyeupe aina ya Toyota Landcruser, likiingia maeneo ya kitongoji hicho, lakini hawakujua kuna nini na linaenda wapi.
“Kwa muda huo hakuna mtu aliyeshughulika na gari hilo, kila mmoja aliona ni kawaida. Kwa hiyo hawakuchukua namba zake za usajili, ila waliona gari jeupe likipita,” alieleza Mtoi.
Alisema asubuhi yake, walishtuka baada ya kuona viroba vimetelekezwa kilomita chache kutoka barabara kuu iendayo Songe, makao makuu ya Wilaya ya Kilindi na Gairo.
“Nilipovisogelea hivyo viroba na kuvifungua, niliona miili ya watu. Baada ya hapo, nilitoa taarifa ofisi ya kata, ambayo nayo iliripoti tukio hilo Kituo cha Polisi Kikunde. Walifika na kushuhudia unyama huo na kwa kuwa hawakufahamika kwenye eneo hilo na la jirani hivyo waliamua kuipeleka miili hiyo katika machimbo ya Seita kwa utambuzi.
“Wale watu walionekana kama wachimbaji na ndiyo maana wakapelekwa mgodini lakini cha ajabu hakuna aliyetambuliwa na ndipo polisi wakaamua kwenda kuihifadhi katika hospitali ya wilaya,” alisema.
Inaporejewa historia ya matukio ya aina hiyo, mwaka 2017, kuliripotiwa nchini matukio kadhaa ya kuonekana maiti za bindamu zikiwa zimefungwa kwenye mifuko ya sandarusi.
Hata hivyo, kipindi hicho miili hiyo ilikuwa inaopolewa ikiwa kwenye mifuko hiyo katika Mto Ruvu mkoani Pwani na baadhi ya fukwe za Bahari ya Hindi mkoani Dar es Salaam.
Katika ufafanuzi wake kuhusu suala hilo, Jeshi la Polisi lilisema lilikuwa linafanya uchunguzi huku likiwaomba watu waliokuwa wamepotelewa na ndugu zao, kujitokeza kupima vinasaba katika jitihada za utambuzi wa miili iliyokuwa inaopolewa.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika tamko lake la Agosti 25, 2017, pia kiligusia suala la kuonekana kwa maiti za binadamu zikiwa ndani ya mifuko hiyo ikielea katika mito na Bahari ya Hindi bila kujulikana ni watu gani na ni nani anayewaua.
Chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake, Anna Henga, kituo hicho kiliitaka Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai kufanya uchunguzi wa miili na matukio hayo ili kutoa taarifa sahihi ambayo ingewatoa hofu wananchi kwa kuwa vitendo vya mauaji ya kinyama dhidi ya binadamu kama hayo ni uvunjifu mkubwa wa sheria na haki za binadamu na Watanzania wana haki ya kufahamu matukio hayo yanafanywa na watu gani.