Mke wa Mrema Afunguka, Awataka Watanzania Kuondoa Hofu



Moshi. Doreen Kimbi, mjane wa aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha TLP, Augustine Mrema amewataka Watanzania kuondoa hofu juu ya hatma ya maisha yake, akisema mmewe alimhimiza kujiamini na kutokuwa na hofu.

Pia, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, viongozi mbalimbali na Watanzania wote kwa ushiriki wao wa karibu baada ya kutokea kwa kifo cha mume wake.

Mrema alifariki dunia Jumapili Agosti 21, 2022 katika Hospitalali ya Taifa Muhimbili (MNH), alipokuwa akipatiwa matibabu na ulizikwa Alhamisi ya Agosti 25, 2022 katika kijiji cha Kiraracha mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne ya Agosti 30, 2022 mjini Moshi, Doreen amesema mume wake alimhakikishia kuwa yupo katika mikono salama hivyo Watanzania wasiwe na hofu juu ya hatma yake.


"Siku zote baba alinihakikishia nisiwe na hofu yoyote kwa maana ninaingia katika mikono salama, sikuwa na hofu yoyote na sikusita kuupokea mkono wake kwenda naye madhabahuni.

Hata baada ya ndoa, alinisisitiza nijiamini na hata pale ambapo yeye hatakuwepo kutoa sauti kusema," amesema Doreen

"Alinihakikishia ndugu zake Profesa Alex Lyatonga Mrema na dada pacha wake Agustina Mrema watasimamia vyema na kunisemea na hata ikibidi kufanya lolote ambalo angeweza kunifanyia, haya ni maneno aliyoniachia rafiki yangu mpenzi,” amesema mjane huyo


Amesema,"yapo yanayosemwa kwa kuyashuhudia kwa macho, ninaamini baba hajafunga macho, kama alivyoniahidi, kuwa hata akifa hatafumba macho, na ninaamini katika maneno yake."

"Sitakuwa na hofu wala sitakuwa na huzuni kwani naamini nimeachwa katika mikono salama. Bado nitaendelea kuishi kwa unyenyekevu, kama niliyekuwa mke wa Mrema, nitaendelea kuwaheshimu na kuwapenda wale ambao niliachwa kwao kama mke wa ndugu yao," amesema

"Nitaendelea kuwa mnyenyekevu kwa Serikali ya Tanzania na Watanzania wote na wote waliokuwa na mapenzi mema na familia ya Mrema" ameeleza

Amesema yapo mengi yanayozungumzwa kuhusu hatma yake akibainisha kuwa yapo baadhi yana ukweli na mengine ni upotoshaji.

"Yapo mengi yanayozungumzwa kwenye vyombo vya habari juu ya hatma ya maisha ya Doreen, yapo ambayo ni ya kweli na hayahitaji uchunguzi wa kiintelijensia na kimaabara."

"Lakini yapo ya upotoshaji kwa sababu ya dhamira mbalimbali nisisitize tu kwa kuwa changamoto zozote zilizotokea na zinazotokea naendelea kuzihifadhi lakini ninaamini mtetezi wangu yu hai” amesema na kusisitiza

“Niendelee kuwahakikishia Watanzania nitamuenzi mume wangu mpenzi na kuishi vile alivyoniasa na kunihusia, muondoe shaka juu yangu ila tumaini langu na imani yangu ni kwa Mungu aliye hai."

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad