Mke wa Mrema, mtoto wafunguka mazito




Dar es Salaam. Wakati Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Augustino Mrema akitarajiwa kuzikwa siku ya Alhamisi kijijni kwake Kiraracha mkoani Kilimanjaro, mkewe Doreen Kimbi amesema amepoteza mume, mpenzi, rafiki, mwalimu na mshauri huku akieleza kuwa alimfia mikononi.

Mrema aliyefariki dunia Jumapili Agosti 21, 2022, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu, ameacha mke na watoto watano.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake eneo la Salasala jijini hapa Doreen alisema atamkumba mumewe kwa mambo mengi, huku akisisitiza alikuwa ni mtu wa karibu sana kwake.

“Amenifia mikononi, namshukuru Mungu kwa maisha aliyompatia hapa duniani na kipindi ambacho nilipata nafasi ya kuwa naye pamoja.


“Nitakumbuka vitu vingi kutoka kwake, siwezi kuvisema kwa sasa, ila yule ni mume wangu, rafiki yangu, mpenzi wangu, alikuwa mshauri na mwalimu wangu, ni vingi ambavyo namkumbuka navyo kwa sasa siko sawa kuongea ila nikikaa vizuri nitaongea na Watanzania,” alisema Doreen.

Hata hivyo, alisema kwa sasa hayuko sawa, hawezi kuzungumza mengi.

“Kwa sasa ninachoweza kusema ni kuwashukuru watu wote waliokuwa wakimuombea mume wangu wakati wa ugonjwa, lakini pia niwashukuru wote ambao mnaendelea kuungana nasi katika kipindi hiki kigumu sana kwetu, naomba tuendelee kumuombea apumzike kwa amani,” alisema.


Alichosema mtoto wake

Wakati mkewe akiyasema hayo, Michael Mrema, ambaye ni mtoto wa tatu kuzaliwa, alisema watamkumbuka baba yao kwa ucheshi wake.

“Baba mara zote alikuwa akitusisitiza kama alikuwa anaacha wosia kwetu na familia kuwa tunapaswa kupendana na kuishi kwa amani siku zote; ni maneno aliyokuwa akiyarudia mara kwa mara,” alisema.

Alipoulizwa ana kumbuka kauli gani ya mwisho ambayo walizungumza na baba yao, Michael alisema;

“Mara ya mwisho tulisali pamoja na kuzungumza naye akiwa mcheshi, lakini aliendelea kusisitiza mambo ya amani kupendana na kuishi salama kama familia moja bila kubaguana.”


Michael alisema baba yao aliwapenda sana aliwaweka karibu sana kwa kuwashirikisha kila jambo alilokuwa akitaka kulifanya.

‘‘Ndiyo maana aliamua kutugawia viwanja karibu na nyumba yake na tumejenga nyumba zetu. Kwa hiyo tukitaka kutoka asubuhi tulikuwa tunapita kumsalimia kabla hatujaenda kwenye shughuli zetu na jioni tukirudi, tulikuwa tunapita pia kumsalimia.”

“Tulikuwa marafiki sana na baba yetu, ni rahisi kuleta wajukuu na akikuita mara moja unakuja kumuona kwa sababu ni karibu tofauti na familia zingine,” alisema.

Hata hivyo, Michael alisema kama familia, hivi sasa wanapita kwenye wakati mgumu sana, kwa sababu ndani ya mwaka mmoja wamepoteza wazazi wote wawili, Agosti mwaka jana walimpoteza mama yao.


Alisema watamkumbuka kwa namna alivyokuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha haki inapatikana.

Alisema pia baba yake alikuwa akipenda wanawe wasome wawe na kazi nzuri ili wajikwamue kimaisha.

Pia, mtoto huyo alisema katika nyanja za siasa baba yake alikuwa nguli kwa sababu alijua mambo mengi kuhusu diplomasia ya siasa.

Jaji Warioba

Miongoni mwa viongozi waliofika nyumbani kutoa rambirambi, ni Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba aliyesema marehemu Mrema atakumbukwa kwa mambo mawili, ikiwamo kuachia nafasi ya uwaziri baada ya kutofautiana na wenzake katika baraza la mawaziri.

Alitaja jingine kuwa atakumbukwa kwa namna alivyoleta upinzani wa kweli wa kisiasa alipohamia NCCR- Mageuzi.


Alisema Mrema ndiye mtu aliyesaidia kuweka msingi wa siasa ya vyama vingi katika nchi na kusisitiza kuwa alipoondoka CCM kwenda upinzani, alitoa upinzani wa kweli na kufanya uchaguzi wa kwanza kuwa wenye ushindani.

“Nafikiri kwa sababu ya uwezo aliokuwa nao na mvuto aliokuwa nao, chama alichokuwa kikiongoza cha NCCR-Mageuzi katika uchaguzi wa kwanza kilipata vitu vingi vya ubunge baada ya CCM,” alisema Warioba.

Maziko

Mrema ambaye alifariki kwa ugonjwa wa mapafu, anatarajiwa kuzikwa katika kijiji cha Kiraracha kilichopo Vunjo mkoani Kilimanjaro, maziko yake yatatanguliwa na ibada ya mazishi itakayofanyika Jumatano Kanisa Katoliki Parokia ya Salasala kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro. Ibada ya mazishi itaambatana na shughuli ya kuuaga mwili.

Msajili wa vyama

Wakati familia ikieleza hayo, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alisema Taifa limempoteza mtu aliyekuwa anatia chachu katika harakati za kisiasa.

Mutungi alisema pamoja na umri wake kuwa mkubwa, dhamira yake ya kweli katika kushirki shughuli za kitaifa ilikuwa wazi.

“Ni hazina ya uzoefu wa masuala ya mikikimikiki ya siasa, tumuombee apumzike kwa amani na mazuri yake tuyaenzi, moja wapo ni kujiamini,”

“Mrema alikuwa mtu wa tofauti, hata watu kumi mkisema hapana katika kitu anachoona anatakiwa kusema ndiyo atasema ndiyo,” alisema Mutungi.

Alisema Mrema alikuwa haogopi mtu pale na alipoona anatakiwa kusimama kutetea kwa maslahi ya watu atasimama na kuzungumza.

“Kuna ule msemo wa ukinizingua na mimi nakuzingua, alikuwa mtu wa hivyo, muwazi na sehemu aliyotakiwa kusema kitu alisema,” alisema Mutungi.

Makala, Gondwe wamlilia

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alisema siasa za upinzani zilizokuwa zikifanywa na Mrema zililenga kuileta nchi pamoja na kuhamasisha umoja.

Alisema: ‘‘Alihamasisha umoja tumepoteza kiongozi mahiri mzoefu mzalendo mwalimu mzuri wa siasa na amefundisha watu wengi mtu ambaye amehubiri umoja na mshikamano.Atakumbukwa kama mtu mpenda maendeleo mdau mzuri na muda wote alikuwa anahamasisha ajengewe barabara ya lami...’’

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe alisema Mrema alikuwa mtu wa kusimamia haki kwa kusikiliza mtu mmoja mmoja.

“Ni mtu ambaye mchango wake katika jamii na Serikali ni mkubwa, kazi alizozifanya zinaonekana,” alisema. Alisema vijana wanaoingia katik siasa wajifunze uzalendo kwani Mrema aliipenda nchi yake na vitu vingi alivyokuwa akizungumza ni vya nchi yake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad