KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi anapiga hesabu ndefu jinsi ya kutoboa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu lakini amegundua winga wake, Bernard Morrison ana tatizo na amemfungia kazi.
KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi anapiga hesabu ndefu jinsi ya kutoboa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu lakini amegundua winga wake, Bernard Morrison ana tatizo na amemfungia kazi.
Kiuhalisia ni kama Nabi haangalii sana mechi dhidi ya Wasudani Kusini, Zalan FC ambao wameomba mechi zao zote mbili zichezwe Dar es Salaam, akili yake iko kwenye mechi ya St.George dhidi ya Al Hilal ambao mmoja wao ana nafasi ya kukutana na Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti ambalo ndilo Gazeti pekee la Tanzania linalouzwa Kenya nzima, Nabi alisema hana presha sana na mechi mbili dhidi ya Zalan akisema kikosi chake kina nguvu kubwa ya kuwatupa nje lakini anahitaji winga aliyetayari katika mechi baada ya hizo mbili.
Nabi ambaye amekwenda Tunisia maramoja, alisema katika maandalizi yao hayo kwasasa wanapambana kuhakikisha Morrison anaimarika zaidi ambapo kama atakuwa tayari kwa asilimia zote watakuwa wameongeza gia ngumu na kubwa kabla ya kukutana na mshindi kati ya St George dhidi ya Al Hilal.
Kocha huyo alisema presha yao iko kwa Morrison na jinsi atakavyoiva katika mazoezi makali yanayoendelea chini ya mtaalam Healmy Gueldich ambaye amemtengenezea programu maalum winga huyo raia wa Ghana aliyewahi kutamba na Simba.
“Tunahitaji kuwa na mawinga walio tayari kiushindani kabla ya kuingia katika hatua ya pili ya mtoano, tatizo bado Morrison hajawa katika kiwango bora ambacho tunakitaka,”alisema Nabi ambaye alimsajili Morrison ili kuongeza kasi kimataifa.
“Sote tunajua kama Morrison akiwa fiti kwa asilimia zote jinsi alivyo hatari,tulihitaji ubora wake huo uanze sasa ili aje kuongeza kitu kikubwa akishirikiana na kina Azizi KI (Stephane) na Mayele (Fiston).
“Bahati mbaya alichelewa kuanza maandalizi ya msimu kuna kazi inatulazimisha kuimarisha sasa katika hizi siku ambazo tutakuwa na mapumziko na sio tu Morrison na wengine wote kwa kuwa tuna ratiba ngumu ya mechi nne katika katika siku 11,”aliongeza Nabi ambaye anaona uzito wa Zalan ni wa kawaida sana kwa Yanga.
WAINGIA MSITUNI
Wakati Nabi akijipanga hivyo kamati ya mashindano ya klabu hiyo yenye vigogo wazito 7 imeingia msituni kuanza kupiga hesabu kuelekea mechi hizo za CAF mapema mwezi ujao.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Mashindano Rodgers Gumbo ameliambia Mwanaspoti kuwa wameanza vikao vizito kwa kupokea mahitaji ya benchi la ufundi kisha wataingia katika kuwaangalia wapinzani wao.
Aidha Gumbo alifichua kwamba uongozi wa Yanga nao kupitia Rais wao injinia Hersi Said uko katika msako wa mtaalam wa siri wa kusoma mchezo ambaye atahitajika katika kuwajua wapinzani wao kazi ambayo itaanzia kwa St.George na Al Hilal.
“Tumeshaanza hayo maandalizi kama kamati tuko katika vikao vyetu, tulihitaji mahitaji ya benchi la ufundi ambayo yameshatufikia na baada ya hapo tunaingia msituni kuanza kazi,”alisema Gumbo.
“Hizi ni mechi ngumu na kuna umuhimu wa kujua ubora wa wale unaokwenda kukutana nao bahati nzuri ungozi wa klabu uko makini sana na unamtafuta mtaalam maalum ambaye ataweza kutupa ubora sahihi wa wapinzani wetu wote tutakaokutana nao lakini pioa makocha wetu wakati huu nao wanapambana katika mambo hayo,”aliongeza.
Hilal au St.George itafuzu kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ambalo ndilo lengo la kwanza la Nabi msimu huu.