Mbeya. Moto umeteketeza magari sita, nyumba nne na pikipiki mbili usiku wa kuamkia leo Jumatatu Agosti 22, huku chanzo kikitajwa kuwa uuzaji mafuta holela katika kata ya Chimala Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.
Imeelezwa kuwa Jeshi la zimamoto na Uokoaji lilifika saa sita usiku na kufanikiwa kuuzima licha ya kuacha hasara kwa mali hizo kuungua.
Diwani wa Kata hiyo, Charles Komba amethibitisha kutokea tukio hilo, akieleza kuwa moto huo ulianza kutokea majira ya saa nne usiku kupitia katika moja ya lori ambalo lilikuwa limeegeshwa katika kituo maalumu cha magari maarufu kama Mama People.
"Ni kweli tukio limetokea lakini tunashukuru baada ya kuwaka moto wananchi walichukua tahadhari na hakuna aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha, Jeshi la Polisi na Zimamoto walifika na kuuzima japokuwa imeathiri mali za watu " amesema Komba.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani Mbarali, Ayoub Sanga amesema taarifa za awali kuhusu chanzo ni biashara holela ya mafuta ya petroli na dizeli iliyokuwa ikifanywa na madereva katika eneo hilo.
Amesema zimamoto walipata taarifa usiku ambapo walifika eneo la tukio na kuanza kuzima moto huo kuanzia saa sita usiku hadi alfajiri na kufanikiwa kuokoa baadhi ya magari na mafuta yaliyokuwa yakiungua.
"Hadi sasa hali ni shwari kidogo kwa sababu tumefanikiwa kuzima moto na kuokoa baadhi ya gari mbili zilizokuwa na mafuta, ila zilizoungua ni sita na pikipiki mbili, niwasihi wanaofanya biashara ya mafuta kiholela waache kwani hata Rais Samia Suluhu amesharuhusu vituo vidogo vya kuuza mafuta maeneo ya vijijini lakini siyo kwa hali hii" amesema Sanga.