MSEMAJI wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema bado wanamshikilia mtoto wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene, huku wakiendelea kukusanya ushahidi kwa hatua za kisheria zaidi.
Misime alisema, kijana huyo James Simbachawene, anakabiliwa na tuhuma za makosa ya usalama barabarani na kusababisha ajali kwa kuyagonga magari mawili.
Akizungumza jana na Nipashe, msemaji huyo alisema hadi jana mchana, kijana huyo alikuwa mahabusu na wanaendelea kukamilisha ushahidi kulingana na watu walioshuhudia tukio hilo ili hatua za kisheria zichukuliwe.
“Kesho (leo) jalada litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ili asome na kuandaa mashtaka kwa ajili ya kumfikisha mahakamani,” alisema Misime.
Juzi vipande vya video fupi vilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimwonyesha James akibishana na polisi wa usalama barabarani baada ya kudaiwa kusababisha ajali kwa kugonga magari mawili likiwamo Toyota Passo yenye namba za usajili T344 DKG na kujaribu kukimbia kisha akakamatwa.
Video nyingine ilionyesha kijana huyo akitoa lugha ya matusi na alipofikishwa kituo cha polisi aliendelea kutoa lugha isiyo ya kistaarabu, alipoulizwa na mmoja wa polisi kituoni alisisitiza juu ya lugha hiyo.
Pia, alionekana akisema yuko tayari kulipa kiasi chochote cha fedha na kutumia lugha isiyo ya kistaarabu dhidi ya waliolalamika kuharibiwa magari yao.
Muda mchache, ulisambaa ujumbe kwenye mitandao ya kijamii unaoelezwa ni wa Waziri Simbachawene ukisema: “Nimeona ‘clip’ (kipande cha video) inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii, nakiri kuwa huyo ni kijana wangu ambaye ni mtu mzima, anajitegemea na ana familia yake.”
“Nimemwagiza Mkuu wa kituo kwa sababu amekosa adabu kwa Jeshi la Polisi na ametenda kosa la usalama barabarani, ashughulikiwe bila huruma kwa mujibu wa sheria, binafsi naomba radhi sana kwa walioathirika na mkasa huo, lakini kwa Jeshi la Polisi na Watanzania wote, poleni kwa usumbufu wowote mlioupata,” alisema katika sehemu ya ujumbe huo ambao ulikuwa na mchanganyiko wa herufi kubwa na rangi mkolezo.
Katika ukurasa wa Twiter mmoja wa wananchi alibandika ujumbe huo na wananchi walitoa maoni yao kuunga mkono andiko hilo:
“Waziri kaupiga mwingi, nilifikiri mara mbili nikagundua huyo ni dogo wala si kijana, kijana mwenye hela na utashi wa wadhifa wa baba yake, alitakiwa suala alimalizie pale pale tena bila hata askari kufika, let us exclude Mr. Minister in this (tumwondoe waziri katika hili).”
Naye, Rugarura aliandika: “Nilichojifunza unaweza tumia muda mrefu na nguvu kubwa sana kujijengea taswira chanya kwa jamii halafu mtu uliyemleta mwenyewe duniani akabomoa kila kitu. Kibaya zaidi jamii bado itakutizama wewe kama ndio ‘failure’ (umeshindwa) kwenye suala la malezi.”
Naye Suleiman Bin Majid, aliandika “Simbachawene katoa kauli nzuri inayomjengea heshima hata yeye mwenyewe.”