KUNA muda mambo mengi ya msingi yanafanywa kwa mzaha sana. Ni kama hili la jezi mpya za Simba. Linachekesha sana.
Katika kuelekea Simba Day, timu hiyo hiyo ilizindua jezi mpya za msimu huu. Jezi ambazo zitavaliwa na mashabiki pamoja na wachezaji. Kusema kweli, ni jezi kali sana. Ni kali kuliko zile za Yanga zilizojaa majengo ya kale.
Lakini ubaya ni kwamba Simba imeleta idadi ndogo sana ya jezi kwa sababu ambazo hazina kichwa wala mguu. Yaani jezi za klabu kubwa kama Simba zikawa zinauzwa duka moja tu nchini.
Yaani kwa kifupi jezi zilikuja chache kuliko uchache wenyewe. Zikauzwa kama nyanya za promosheni. Zikamalizika ndani ya saa chache tu.
Huu ni uzembe uliopitiliza. Hakuna biashara ya hivi. Unawezaje kuleta jezi chache kihivyo kwa timu kubwa kama Simba.
Wanadai kuwa wamechelewa kwasababu ya mdhamini mpya. Vipi kuhusu Yanga? Mbona wamewahi na walikuwa na mdhamini mpya.
Simba ilishatambua mapema kuwa itakuwa na mdhamini huyo. Ilikwenda kwenye maandalizi ya msimu mpya Misri ikifahamu mdhamini mpya ni nani. Nini kilikwama? Ni uzembe tu wa watendaji.
Kuna watu wametumia nguvu kubwa sana kuijenga hii biashara ya jezi, lakini watu wachache kwa uzembe wao wanataka kuishusha. Hii haijakaa sawa.
Simba inapaswa kuwa makini na hili, vinginevyo itapata shida kuisimamisha tena biashara ya jezi hapo baadaye.