YANGA imezindua jezi rasmi za mashindano msimu wa 2022/23. Ni msimu wa nne sasa Yanga imekuwa ikifanya hivyo baada ya kuingia mkataba na GSM Sports kwa ajili ya mauzo hayo.
Ni wazi katika miaka hii minne kazi kubwa imefanyika katika ubunifu wa jezi. Kazi kubwa imefanyika pia kuwafanya mashabiki wawe na utamaduni wa kuvaa jezi mpya kila msimu.
Si jambo rahisi hata kidogo, hasa katika nchi masikini kama hii kuwashawishi watu wanunue jezi mpya kila msimu.
Lakini sasa kwa Tanzania imewezekana. Watu wanaona fahari kuvaa jezi za klabu anayoipenda.
Yanga walichelewa kidogo kuanza biasha hii, wakati wenzao Simba walianza mapema.
Ni kama miaka zaidi ya 10 Simba imekuwa na utamaduni wa kuzindua jezi mpya kila msimu.
Yanga walichelewa sana. Labda kwasababu ya uwepo wa Bilionea Yusuf Manji ambaye alikuwa anatoa pesa ya kila kitu pale Yanga.
Ndio maana walianza biashara hii miaka mitatu nyuma.
Ila, tukubali tukatae watu wa Yanga sasa wananunua jezi zao kwa wingi sana, pengine kuliko hata mashabiki wa timu nyingine.
Angalia kilichotokea mara tu baada ya uzinduzi. Mashabiki wa Yanga walifurika kwenye maduka kama siafu. Kila mtu anataka jezi mpya. Inafurahisha sana.
Hata hivyo, swali la msimu ni je Yanga inanufaikaje na biashara hiyo ya jezi? Hapa ndio penye shida kidogo.
Wenzao Simba walishapiga hatua kwenye hilo. Simba wanapata Shilingi 1 bilioni kwa mwaka kutoka kwa Vunjabei. Mauzo ya jezi atajua mwenyewe, lakini mzigo lazima utoke.
Huu ndio mkataba mkubwa zaidi wa jezi kuwahi kutokea nchini. Lakini Simba waliweka nguvu na juhuzi zao kufika hapo.
Yanga wanapata nini? Bado haijaeleweka vizuri. Kwa mujibu wa mkataba wa kwanza na GSM Sports, Yanga inapata Sh1,300 kwenye kila jezi moja inayouzwa.
Yaani jezi moja ya Yanga sasa imefikia Sh35,000, lakini ikiuzwa ni Sh1,300 inaingia klabuni. Inachekesha sana. Ni biashara gani ya hivi?
Mtu anayenunua jezi kwa bei ya Jumla anauziwa Sh28,000, yeye anakwenda kuuza 35,000. Anapata faida ya Sh7000 kwa kila jezi moja lakini Yanga ambayo ndio yenye nembo ya jezi hiyo inapata 1,300. Kweli? Kuna kitu hakipo sawa mahala.
Niliona kwenye hesabu za mapato na matumizi ya Yanga kwa mwaka jana, marabaha wa jezi kwa mwaka haukuwa umefika hata Milioni 200. Kweli?
Yaani Yanga ilipata fedha nyingi kwenye watu waliolipia APP yao kutazama habari, kuliko mgawo waliopata katika mauzo ya jezi. Ni ajabu na kweli.
Ni lazima iwe wazi kuwa Yanga itapata kiasi gani cha fedha kwa mwaka kutokana na mauzo ya jezi. Anayefanya biashara hiyo atajua anakwenda kufanya nini kurejesha fedha zake. Lakini Yanga ijue kabisa inapata nini.
Lakini kama bado inapata Sh1300 kwenye mauzo hayo, huo ni mkataba wa kinyonyaji.