Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa
Moshi. Jeshi la polisi Mkoani Kilimanjaro linamshikilia Jonas Mushi (26) mkazi wa kijiji cha Manushi kati Wilaya Moshi, kwa tuhuma za kwa kuwauwa kwa kuwakata panga watu wawili ambao ni mke na mume kutokana na imani za kishirikina.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kwamba yalitokea Julai 19 , 2022 majira ya saa 17:45 jioni, ambapo amesema mtuhumiwa aliwakatakata kwa panga Paul Mushi (70), Felista Mariki Mushi (65), ambao ni mke na mume hadi kupoteza maisha kwa madai kuwa wamekuwa wakimloga.
Kamanda amesema mtuhumiwa alifika kijijini hapo jana akitokea Kibaha mkoani Pwani na alipofika nyumbani alichukua panga na kuelekea nyumbani kwa baba yake mkubwa ambae ni marehemu.
“Mtuhumiwa alipofika nyumbani kwa marehemu, alianza kumshambulia kwa kumkatakata sehemu mbalimbali za mweli hadi kupoteza maisha.
“Wakati akifanya kitendo hicho mke wake ambae ni marehemu alimkuta mtuhumiwa akimshambulia mume wake na kujaribu kumsaidia ndipo mtuhumiwa alipoanza kumshambulia na kumkatakata kwa panga hadi kupoteza uhai," amesema.
Kamanda amewataka wananchi kuacha imania potofu za kishirikina na kwamba serikali haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakaye jichukulia sheria mkononi.