Nyumba za kupanga zinavyoharibu akili



 
Dar es Salaam. Kama unaishi nyumba za kupanga zenye masharti lukuki hii inakuhusu sana, wataalamu wa afya ya akili na wanasaikolojia wameonya kuwa masharti hayo ni moja ya kichocheo cha mtu kukumbwa na magonjwa ya afya ya akili ikiwemo sonona.

Takwimu za magonjwa ya afya ya akili kwa mwaka jana kutoka Wizara ya Afya zinaonyesha Watanzania milioni saba wana matatizo ya afya ya akili, huku Mkoa wa Dar es Salaam ukionekana kinara na idadi kubwa ya watu wenye matatizo hayo.

Kauli ya wataalamu hao inakuja wakati Debora Maiko mkazi wa Mbezi Afrikana Dar es Salaam, akisimulia mama mwenye nyumba wake kumkataza kuamka alfajiri kabla yake na wakati mwingine haruhusiwi kutoka ndani hadi mama huyo amwage maji barazani.

Akizungumza hivi karibuni na Mwananchi Debora alisema jambo la ajabu katika mkataba mama huyo hakuainisha masharti hayo, pia hakuna mpangaji anayeruhusiwa kupiga nyimbo za dini au kutoka nje kabla ya mama huyo kuamka.


 
Alisema kunapotokea hali ya kukiuka utaratibu huo, mwenye nyumba hutishia kusitisha mkataba kwa madai kuwa mtenda tukio anamuharibia mambo yake.

Kauli ya Debora ianungwa mkono na Sophia Urasa mkazi wa Mabibo anayeshangazwa na masharti ya jirani yao asiyepangisha vijana waliooa ndani ya nyumba yake au familia yenye mtoto mchanga kuishi kwake.

Daktari Idara ya Afya ya Akili, kutoka Hospitali Rufani Kanda ya Mbeya, Dk Raymond Mgeni alisema vitisho na masharti kandamizi anayotoa mmiliki wa nyumba kwa mpangaji wake humsababishia mpangaji kupata msongo wa mawazo ambao huchangia mtu kuingia katika kundi la magonjwa ya akili ikiwemo sonona.


“Mwenye nyumba anapoweka masharti magumu bila kufahamu aina ya watu anaowapangisha aidha ni wanafunzi, mtu mwenye kipato chenye kutia shaka, anayepitia changamoto ya mahusiano au kodi kwa pamoja vinamuingiza mtu huyo katika sonona,’’ alisema.

Alisema athari ya mtu kupata msongo wa mawazo ni kuharibu utendaji kazi ikiwamo kuchangamana na watu, hali inapokuwa mbaya zaidi mhusika anaweza kuchukua uamuzi mgumu ikiwemo hata kukatisha uhai wake.

Dk Mgeni alishauri ni vyema wapangaji kutokimbilia nyumba hizo na badala yake wahakikishe masharti yaliyopo ni rafiki kwao.

Akilizungumzia hilo mwanasaikolojia, Ramadhani Masenga kutoka taasisi ya Mental Hygine Instute ya Dar es Salaam, alisema binadamu kwa asili ni kiumbe mwenye shauku na kupenda uhuru wake.


 
Alisema masharti yanayowekwa katika nyumba za kupanga wengi wanayakubali si kwa sababu wanayaridhia bali hawana cha kufanya kwa wakati huo.

Athari inakuwa hivi: “Kama umekubali kuishi katika nyumba yenye masharti makubwa na wewe unataka kuwa na uhuru na kawaida binadamu ni kiumbe mwenye shauku, anapoambiwa asitoke alfajiri kabla ya mwenye nyumba basi hii kitu itamsumbua kwa muda kwenye akili yake.

“Kitendo cha kumwambia asitoke muda huo unamtengenezea maswali na shauku ya kutaka kujua kwa nini asitoke muda huo, hivyo kuna wakati atataka kutoka ili kuona kilichopo na hata asipoona kitu ataendelea kuweka akili akitaka kufahamu zaidi. Hii hali itamtafuna kwa miaka mingi hata kama ameondoka kwenye nyumba hiyo bila yeye kufahamu,” alisema.

Masenga alisema kuna wakati mtu hukosa furaha bila kutambua kwa nini yupo kwenye hali hiyo.


“Anajiuliza ana deni? hana, amefiwa wala hajafiwa lakini kwa nini hana furaha hivyo hivi vitu vidogo vidogo vinamsumbua mtu kiasi cha hata kukosa hamu na kupoteza msisimuko katika maisha,” alisema Masenga.

Hata hivyo, aliongeza kuwa japo mtu anayeishi katika nyumba za kupanga yenye masharti kandamizi ataonekana yupo huru, lakini kichwani anakuwa yupo gerezani na vitu anavyoviwaza vitaendelea kumtafuna bila kujua cha kufanya.

“Mtu kukumbwa na hasira za ghafla japo zipo sababu nyingine kwa kuwa yapo masharti mengine yanachochea hasira kwa kiwango kikubwa na hapo ndipo maamuzi magumu hufanyika.

“Chochote anachofanyiwa binadamu au anachokiona kikifanyika kinakwenda kuongeza jambo katika hisia zake, masharti kama hayo yanamfanya mtu apoteze kiwango chake cha furaha na ucheshi wake wa kawaida,” alisema.

Ushuhuda nyumba za kupanga

Mkazi wa Mbagala Kizuiani, Dar es Salaam, Jackson Komba anaelezea adha za kuishi na mwenye nyumba katika eneo moja.


 
Alisema changamoto ni nyingi kwa wapangaji wanaoishi nyumba moja na mmiliki ikilinganishwa na wale anaoishi mbali na mwenye nyumba.

“Changamoto kubwa kwangu ni namna ambavyo naendesha maisha yangu, mimi sijaoa na nina tabia ya kutengeneza mlo wangu nyumbani na kiukweli napenda kula vizuri maini, mbogamboga, chakula kizuri. Sasa ninapokuwa naandaa masotojo yangu mwenye nyumba anaona na hafurahii ile hali,” alisema.

Alisema kwa kuwa mpangaji anavaa vizuri na kula vizuri muda wa kulipa kodi unapofika asipolipa kwa wakati ugomvi mkubwa huzuka ukiambatana na kauli za dharau.

“Mtu anakwambia unakula na kuvaa vizuri lakini kodi hulipi kwa wakati, sasa hayo ni mambo ya maisha yangu,” alisema.

Alitaja adha nyingine kuwa ilimlazimu aingie katika uhusiano asioutarajia kutokana na vishawishi vya watoto wa mwenye nyumba na ndugu zake.

“Alikuwa na ndugu wasio na kazi pale nyumbani. Kwanza watoto wake wawili wa kike nilijikuta nimekuwa nao katika mahusiano bila kutarajia. Baadaye wakaja watoto wa ndugu zake kisha wifi yao japo haikuwa dhamira yangu ila vishawishi ni vingi,” alisema.

Alipoulizwa kwa nini alifanya hivyo, Komba alisema walikuwa wakimfuata ndani kwake na kumshawishi kwa tamaa wakiamini ana uwezo mkubwa kifedha.

Alitaja adha nyingine kuwa ni kukosa uhuru, “Pale kulikuwa na geti na funguo moja kuna siku nilichelewa kufika geti limefungwa wote wamelala, nilipata shida nimgongee nani, baadaye niliamua kutafuta fundi nikabadilisha kitasa na kutengeneza funguo nyingi nikagawa kwa kila mmoja.”

Komba alisema haikuishia hapo anapambana na suala la usafi ambalo inamlazimu kufagia na kupiga deki chooni.

“Mimi mtoto wa kiume unataka nishike ufagio kweli? Ilibidi niajiri mtu anakuja kufanya usafi kila zamu yangu inapofika. Lakini, hata hilo kuna wakati alikataa mtu asionekane nyumbani kwake,” alisimulia Komba.

Andrea Joseph aliyewahi kuishi Tabata Kisiwani alielezea namna ambavyo alikuwa kwenye wakati mgumu kutokana na mama mwenye nyumba, ambaye alikuwa na mabinti wawili kutohitaji mwanamke mwingine kumtembelea.

“Yule mama alinionya kuwa kama nataka kuishi kwake basi asione mgeni wa kike kwangu na kuna wakati alikuja dada yangu ikawa kosa kubwa. Alinisema sana na kuniambia nihame kwake kwa sababu namkosesha raha na mabinti zake,” alisema.


 


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad