MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Taisi Kata ya Bumera, mkoani Mara, Ibrahimu Maryoba, amefariki dunia kutokana na shinikizo la damu wakati akienda kuamua ugomvi wa jirani yake.
Akizungumza na Nipashe kuhusu tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Sokoni, Moi Buruma, alisema majira ya usiku akiwa nyumbani kwake Kitongoji cha Nyairoma, Ibrahimu alikwenda kuamulia ugomvi kwa jirani yake aliyetajwa kwa jina moja la Juma aliyekuwa na ugomvi na mke wake.
Mwenyekiti huyo alisema jirani yake alipiga kelele za kuomba msaada, ndipo mwalimu huyo alipotoka na kwenda kuamua ugomvi huo na alipofika nje alianguka na kupoteza fahamu.
Alisema wasamaria wema walijitokeza na kumbeba kumpeleka Kituo cha Afya Sirari kwa ajili ya kupata matibabu, lakini alifariki wakati akihudumiwa.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum Tarime Rorya, ACP Geofrey Sarakikya, alisema: “Ni kweli kumetokea kifo cha mwalimu huyo na taarifa za mganga zinaonyesha alifariki kutokana shinikizo la damu, mishipa ya damu ilipasuka na kuvuja kwa ndani na kusababisha kifo chake.”
“Tunaendelea na uchunguzi zaidi na tunawaomba wananchi kuacha kueneza mambo yasiyo na uhakika badala yake wafuate mambo ya kitaalamu kama anavyoeleza mganga wa kituo cha afya kwamba mwalimu huyo alifariki kutokana na shinikizo la damu.”
Mwili wa mwalimu huyo ulipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Tarime kufanyiwa uchunguzi, ulirejeshwa nyumbani kwake katika Kitongoji cha Nyairoma, Kijiji cha Sokoni na unatarajiwa kuzikwa leo.