Rombo. Mwanafunzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI), Hombolo mkoani Dodoma, Lightness Shirima (22) amesema anahangaika kulipa deni la matibabu la Sh9 milioni aliloliacha baba yake aliyefariki dunia Hospitali ya Mloganzila ili apatiwe kitambulisho chake cha uraia (Nida).
Lightness, ambaye anasoma chuoni hapo mwaka wa pili LGTI, alisema hivi karibuni kuwa baba yake, Priscus Shirima alifariki dunia Julai 4, mwaka huu katika hospitali hiyo jijini Dar es Salaam baada ya kulazwa kwa siku 40 na kuacha deni.
Ili kuwa na uhakika deni hilo litalipwa, uongozi wa hospitali hiyo unadaiwa kumtaka mwanafunzi huyo kutoa kitambulisho cha Nida kama dhamana na kupewa mwili wa baba yake kwa sharti la kulipa Sh50,000 kila mwezi.
“Sielewi nitasoma au nitaenda kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa gharama za hospitali, najua hali niliyonayo ni ngumu sana, hapa nilipo sijui nitaishije maana tumeachwa yatima na ndugu zetu hawana uwezo kutusaidia,” alisema Lightness.
Uongozi wa hospitali hiyo ulikiri kuidai familia hiyo Sh9 milioni gharama za matibabu mgonjwa kukaa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwa siku 40 mfululizo.
Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Neema Mwangomo alisema, “huyu mgonjwa alikaa ICU mwezi mmoja na kama siku 10, ndio maana gharama zimekuwa kubwa, lakini ofisi ina utaratibu kama mtu hana uwezo kuna taratibu angepaswa afuate ili kupunguziwa gharama au kusamehewa.
“Kilichofanyika baada ya kufariki dunia, ndugu zake walikuja na wakasema hawana uwezo na sisi kweli tukawapatia mwili kwa sababu hatukai na mwili tunathamini utu, kwa hiyo tuliwapa mwili ili kwenda kufanya taratibu za maziko na tukaingia makubaliano na ndugu ya kulipa zile gharama,” alisema Mwangomo.
Kuhusu hospitali kuchukua kitambulisho cha Nida cha mwanafunzi huyo, Mwangoma alisema aliacha namba zake za Nida ili waweze kupewa mwili wa marehemu kwa kuwa walikuwa hawajalipa gharama za matibabu za hospitali.
“Ikitokea ndugu wamekuja kuchukua mwili na akatokea mtu mmojawapo ana namba ya Nida anaacha kitambulisho chake wanapewa mwili wanaenda kuzika. Hospitali ina utaratibu wake maana sisi tunachoangalia ni utu kwanza,” alisema Mwangomo.
“Kama familia imekwama wanaweza kurudi ofisini nafasi ipo wazi. Kama kuna lolote lile arudi atueleze ili kuona tunafanyaje, lakini ni kweli tunadai familia Sh9 milioni.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti, Lightness alisema baba yao aliugua shinikizo la damu ambalo lilimpelekea kupofuka macho na kupata kiharusi.
Alisema anapaswa kulipa deni la baba yake katika hospitali hiyo licha ya kwamba bado ni mwanafunzi na kuiomba Serikali impe msamaha wa deni hilo kwa kuwa hana uwezo wa kulilipa.
Alisema baada ya baba yake kufariki, familia walitaka kuchukua mwili na kwenda kuuzika nyumbani kwao Rombo, mkoani Kilimanjaro, lakini walikuta deni la Sh9 milioni ambalo hawakuwa na uwezo kulilipa.
Lightness alisema uongozi wa hospitali ulimtaka atoe kitambulisho chake cha Nida ikiwa ni dhamana ya kukomboa mwili wa baba yake ukazikwe.
Alisema baada ya kutoa kitambulisho alipewa masharti kuwa kila mwezi anapaswa kulipa takribani Sh50,000 ili kupunguza gharama alizokuwa anadaiwa baba yake huyo wakati akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo kwa siku hizo 40.
“Baada ya baba kufariki dunia nilishindwa nifanyeje maana sina msaada na familia yangu ni duni, nilifanya jitihada zote za kuomba mwili wa baba yangu nikauzike lakini niliambiwa mpaka nilipe gharama za matibabu alizokuwa anadaiwa.”