Mwenyekiti wa jamii ya Wahadzabe, Bunga Paulo akizungumza kwa niaba ya wenzake
HATIMAYE jamii ya kabila la Wahadzabe leo tarehe 23 Agosti, 2022 wamekubali kuhesabiwa baada ya kupatiwa nyama pori na matunda kama walivyokuwa wameomba hapo awali wakati serikali ikijiandaa na zoezi la sensa ya watu na makazi. Anaripoti Helena Mkonyi, TUDARCo… (endelea)
Hayo yamejiri wakati Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela alipoungana na timu ya makarani na waratibu wa zoezi hilo la sensa kuitembelea jamii hiyo ili kujionea namna walivyoitikia wito wa Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki kikamilifu zoezi hilo.
Mongela amesema waadzabe bado wako katika hatua za mwanzo za ujima na wanategema na matunda mwitu ili kujipatia chakula.
“Kwa sababu ndugu zetu hawalimi lakini pia wanaishi kwa kuhama hama kutoka sehemu moja hadi nyingine, ndio maana serikali iliandaa mazingira maziru ikiwamo kuwagawia nyama kama ambavyo walivyoomba, tumewaletea nyama ya mbogo, pundamilia na matunda mbalimbali kama vile ndizi.
Mwenyekiti wa jamii ya Wahadzabe, Bunga Paulo ambaye pia ni msemaji wa jamii hiyo y amesema wapo tayari kuhesabiwa na wanafuraha kubwa kuhesabiwa katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
Naye Mratibu wa sensa wilaya ya Karatu kata ya Baray, Rosemary SSamson amesema kwamba wilaya ya Karatu iliandaa mazingira maalumu kwa ajili ya kuwahesabu Wahadzabe ndio maana zoezi hilo linaendelea kufanyika kwa ushirikiano na muitikio mkubwa.