MSIMU wa 2011/2012, mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi aling’ara sana tangu alipotua Tanzania mwaka 2009. Alimaliza Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 12 yaliyoambatana na kiwango cha juu kwenye mashindano ya ndani hadi ya nje.
Entente Sportive Setifienne au maarufu kama Entente de Setif hawatamsahau kwa bao la dakika ya mwisho lililowatupa nje ya Kombe la Shirikisho Afrika. Raia huyo wa Uganda, alifunga bao hilo kutokana na uwezo wake binafsi. Aliwapunguza baadhi ya wachezaji wa timu pinzani akiwa nje ya 18 na kupiga shuti kali lilimshinda kipa na kwenda moja kwa moja wavuni. Bao hilo liliifanya Simba kusonga mbele pamoja na kufungwa mabao 1-3 kwani nyumbani ilikuwa imeshinda 2-0. Bao hilo likaingia kwenye kinyang’anyiro cha CAF kuwania bao bora la msimu, lakini halikushinda.
sakho pic 1
Emmanuel Okwi
Baada ya msimu huo, Okwi akaenda kwenye majaribio nchini Austria katika timu ya RB Salzburg. Mwaliko huo haukuja tu kutokana uwezo wake, bali pia ‘connection’ kutoka kwa nahodha wa Timu ya Taifa ya Uganda wakati huo, Ibrahim Sekagya ambaye pia alikuwa nahodha wa RB Salzburg.
Okwi alitakiwa kufanya majaribio kwa wiki mbili, lakini baada tu ya siku tatu akaanza kusumbua anataka kurudi nyumbani.
Alipokuwa akisisitizwa kupambana ili atoboe, akasema anaumwa na hawezi kuendelea na majaribio. Akaruhusiwa kuondoka na hadithi yake ikaishia hapo.
Lakini hadithi ya RB Salzburg haikuisha. Baada ya kumkosa Okwi wakamuita kijana mwingine kutoka klabu ya Metz iliyokuwa Ligi Daraja la Pili nchini Ufaransa kufanya majaribio. Kijana huyo mzaliwa wa Bambali, Senegal akaitumia nafasi hiyo vizuri akatoboa.
Kijana ninayemzungumzia hapa ni Sadio Mane ambaye kwa sasa ni nyota mkubwa sana duniani. Julai mwaka huu, Sadio Mane alikuwa jukwaa moja na nyota wa Simba, Pape Ousmane Sakho kwenye Tuzo za Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF). Mane alikuwa akiwania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika na Sakho alikuwa anawania tuzo ya bao bora la msimu barani Afrika.
Wote wawili walishinda tuzo zao na baada ya hapo wawili hao wamekuwa na mawasiliano ya karibu. Wiki iliyopita walikuwa na mazungumzo mafupi kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo Mane alimwambia Sakho anamfuatilia kwa karibu.
Kilichofuata baada ya hapo ni taarifa za Mane kumtafutia Sakho nafasi kwenye klabu ya RB Salzburg ambayo yeye alipitia, lakini nyota mwingine wa Simba alishindwa.
Kama hii itakuwa kweli, basi ile nafasi ambayo Simba iliikosa mwaka 2012 kwa nyota wao kwenda RB Salzburg inaweza ikapatikana mwaka huu, miaka 10 baadaye. Kila kitu kinawezekana!