KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasredine Mohammed Nabi amelilalamikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi kutokana na ratiba yao ya Ligi kuwabana wachezaji kiasi cha kukosa muda wa kutosha wa kupumzika.
Nabi raia wa Tunisia ambaye ameiongoza Yanga kutwaa mataji matatu msimu uliyopita amesema hayo mara baada ya kurejea Kambini, Avic Town ambako timu yake inajiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC.
“Kikosi changu nimekikuta kiko vizuri, wachezaji wote wana fitness ya hali ya juu hata wale wageni pia fitness yao iko vizuri. Niliwapa wachezaji wangu programs maalum za kufanya wakati wakiwa mapumziko ili wakirejea kambini, fitness yao isishuke.
Baadhi ya nyota wa Yanga waliokuwa Timu ya Taifa, Taifa Stars wamekosa muda wa kupumzika kulingana na msongo wa ratiba
“Jambo linalonisumbua ni ratiba ya TFF, kwa kawaida duniani kote inatakiwa baada ya msimu wachezaji uwape siku 20 za mapumziko ambapo hawatafanya jambo jingine zaidi ya mapumziko, hawatakiwi kabisa kuwaza mambo ya mpira kwa wakati huo.
“Baada ya hapo timu inatakiwa ipate preseason ya wiki sita, lakini ukiangalia ratiba ya TFF, kuanzia mechi ya mwisho ya Kombe la Shirikisho, Julai 2, 2022 mpaka mechi ya Ngao ya jamii ni wiki sita tu, utafanya mazoezi siku ngapi na likizo itakuwa siku ngapi?
“Tunaomba TFF ifanye mpangilio vizuri wa likizo na kuipa timu muda mzuri wa maandalizi, hii itasaidia hata wachezaji wa ndani, mfano Tanzania kuna wachezaji wazuri kama Feisal na Dickson Job, hawajapata muda mzuri wa kupumzika sababu walikuwa timu yaTaifa, TFF wangebadilisha tarehe ya kuanza ligi, itasaidia hata timu nyingine, sio Yanga pekee,” amesema Nabi.