IKIWA zimebaki siku nne raia wa Kenya kuingia katika vituo vya kupigia kura katika uchaguzi mkuu, kampeni zinazidi kuchanja mbuga katika maeneo mbalimbali ndani ya taifa hilo.
Katika nafasi ya juu ya urais, wagombea wanne wanapigana kufa na kupona kupata ridhaa ya kukalia kiti hicho huku vumbi likizidi kumtimka kati ya kambi mbili hasimu. Wagombea hao ni Raila Odinga kutoka muungano wa Azimio la Umoja Kenya, naibu rais William Ruto anayewania kupitia tiketi ya chama cha UDA, George Wajackoyah na David Mwaure wa chama cha Agano.
Hata hivyo, Odinga na Ruto wameonekana kukabiliana ipasavyo kwa kuwa kila mmoja anaonyesha nguvu zake za kisiasa kwa kufanya kampeni zitakazohakikisha anaingi Ikulu.
Wagombea hao wamekuwa kivutio cha maelfu ya watu kwenye mikutano yao ya mwisho ya kampeni.
Wakati watu wanazidi kuwaangazia wagombea hao, nyuma yao kuna wanawake ambao ndio wanahakikisha wagombea hao wanendelea kupambana.
Mmoja wa wagombea hao wanne endapo akishinda, kuna mwanamke ambaye atakua ‘festi ledi’ au mama wa taifa la Kenya kwa miaka mitano baada ya Margaret Kenyatta kuaga Ikulu ya Nairobi.
Je ni nani kati ya wanawake hawa wanne atachukua nafasi hiyo ambayo ni muhimu nchini Kenya?