OFISA wa Polisi aliyekuwa katika Kituo cha Polisi Mburahati, Dar es Salaam, Inspekta Festus Simon, ameieleza Mahakama jinsi alivyoweka mtego wa kumkamata mfanyabiashara wa meno ya tembo kwa kujifanya anataka kununua jino moja kwa Sh. 150,000.
Inspekta Simon amedai kuwa aliweka mtego huo baada ya msiri wake kumpa namba ya simu ya mshtakiwa, Hassan Abdallah, huku akimrubuni kuwa anafanya biashara ya meno ya tembo.
Simon alitoa madai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Evodia Kyaruzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati akitoa ushahidi dhidi ya Abdallah. Inspekta Simon alidai kuwa, kwa sasa yupo Kituo cha Polisi Bunda mkoani Mara anapofanyia kazi.
Alidai Januari 3, 2019 akiwa ofisini kwake, alipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna mtu anafanya biashara ya meno ya tembo na anatafuta mnunuzi wa vipande vinane.
"Msiri alinipa namba ya simu ya Abdallah nikaanza kufanya naye mawasiliano nikijitambulisha kuwa mimi ni mfanyabiashara nataka kununua meno ya tembo," alidai Inspekta Simon.