ENEO la kiungo linategemewa kunogesha pambano la Ngao ya Jamii litakalozikutanisha timu za Simba na Yanga leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Uwepo wa idadi kubwa ya wachezaji wa nafasi ya kiungo waliopo katika vikosi vya timu hizo unatarajiwa kuwa chachu ya kuzisaidia timu zao kusaka matokeo mazuri katika mechi hiyo.
Uwezo binafsi wa wachezaji wengi wa nafasi ya kiungo waliopo katika vikosi vyao lakini pia utekelezaji mzuri wa maagizo ya benchi ambao wamekuwa nao hapana shaka utaifanya mechi hiyo kuwa na mvuto wa kipekee katika dakika zote 90.
Kwa upande mwingine mashabiki wa soka watakuwa na fursa ya kuona ushindani wa viungo hao kutegemeana na nafasi zao watakazopangwa katika mchezo huo uliopangwa kuanza saa 1:00 usiku.
Aziz Ki v Nelson Okwa
Mafundi wawili wa kuchezesha timu ambao Yanga na Simba zimewanasa katika dirisha linaloendelea la usajili watakuwa na kibarua cha kuonyesha nani kiboko zaidi ya mwenzake.
Aziz Ki aliyesajiliwa na Yanga kutokea Asec Mimosas ya Ivory Coast na Nelson Okwa ambaye Simba imemchukua kutoka Rivers United ya Nigeria wote wana sifa zinazoshabihiana za unyumbufu, kasi na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira.
Mbali na hilo, wote wawili ni hodari wa kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao lakini pia huwa na maamuzi ya haraka pindi wawapo na mpira miguuni.
Feisal Salum v Clatous Chama
Uwezo mkubwa wa Feisal Salum ni kupiga mashuti ya mbali lakini pia kuchezesha timu akibebwa na pasi zake ambazo hufikia walengwa kwa usahihi.
Kwa upande wa Simba wana Clatous Chama ambaye anasifika kwa kuchezesha timu, kupiga pasi za mwisho na kufunga mabao.
Salum Abubakar v Sadio Kanoute
Viungo wawili wanaocheza mbele kidogo ya viungo wa ulinzi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kwa Yanga na Sadio Kanoute watakuwa na jukumu kubwa la kuunganisha timu katika mechi hiyo.
Kanoute anamudu vyema kutoa sapoti kubwa pindi timu inaposhambuliwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupora mipira na kuziba mianya.
Kwa upande wa Sure Boy yeye amekuwa
na mchango mkubwa pale timu inaposhambulia kutokana na uwezo wake wa kupiga pasi zinazofikia walengwa kwa usahihi lakini pia kufungua ukuta wa timu pinzani.
Jonas Mkude v Khalid Aucho
Viungo wawili wa ukabaji, Jonas Mkude (Simba) na Khalid Aucho (Yanga) watakuwa na kibarua cha kuhakikisha safu zao maeneo ya ulinzi zinakuwa salama.
Wote wawili japo hawana kasi ni hodari wa kuziba mianya kwa wapinzani pindi wanaposhambuliwa, lakini wana uwezo wa kuchezesha timu kuanzia nyuma.
Uwepo wao uwanjani huwapa kazi rahisi viungo wa ushambuliaji wa timu hizo kutokana na pasi zao ambazo huvunja mistari ya viungo wa timu pinzani.
Misimu miwili iliyopita eneo hilo la viungo ndilo lililoamua mechi baada ya Zawadi Mauya kufunga bao kwenye mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya 2020-2021, kisha Taddeo Lwanga aliyetemwa na Simba kufunga kwenye fainali ya ASFC ya msimu huo uliyopigwa Lake Tanganyika, Kigoma kabla ya Feisal Toto, kutupia katika nusu fainali ya ASFC iliyopita iliyopigwa CCM Kirumba, Mwanza.