Chamwino. Mzazi aliyepokea mahari ya kumuoza binti wa miaka 15 ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Sekondari ya Makang’wa, ametemeshwa tonge mdomoni.
Ng’ombe wanne na mbuzi kati ya sita hadi nane walitolewa kwa ajili ya ndoa hiyo, huku kukiwa na deni lililobaki ili kumbeba jumla binti huyo.
Ndoa hiyo ya kimila ilikusanya watu wengi, ikisindikizwa kwa ngoma na vyakula kemkem.
Yohana Mhanjilwa (64), mkazi wa Kitongoji cha Mabwe kilichopo Makang’wa wilayani Chamwino alikamatwa wakati sherehe zikiendelea pindi askari polisi walipoivamia ghafla na kuwatia mbaroni wahusika.
Binti huyo alikuwa akiozeshwa kwa kijana mwenye umri wa miaka 17 kutoka Kijiji cha Mvumi akielezewa kuwa anajitambua na ana ari ya kujenga familia imara.
Mkuu wa Sekondari ya Makang’wa, Jilly Nindi alikiri kumtambua binti huyo aliyepangiwa kuanza kidato cha kwanza Januari mwaka huu, lakini hakuripoti shuleni na taarifa za utoro huo zilishapelekwa kwa mamlaka husika.
Nindi alisema ilimchukua muda mrefu kumtafuta mtoto huyo ili aripoti shuleni lakini hakumpata, ndipo akatoa taarifa kwa ofisa mtendaji wa kata kwa hatua zaidi akiwekwa kwenye kundi la watoro.
“Binafsi sikuwa na cha kufanya, kama unavyojua wanatoka shule ya msingi mimi siwafahamu, lakini jina la Rehema Ndahani nalikumbuka na ni miongoni mwa niliowatolea taarifa za utoro, kwa hiyo hayo mengine nashangaa kusikia kuwa amekuwa mke wa mtu,” alisema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Makang’wa, Ibrahimu Athuman alikiri kupokea taarifa za binti huyo lakini akasema hawezi kulizungumza zaidi.
Hata alipoulizwa kama anajua kuwa mtoto huyo anaolewa kwa sherehe kubwa kijijini hapo bado alikataa kuzungumza, akisema ni mambo yaliyo juu ya uwezo wake, ingawa katika eneo la tukio alikuja akiwa amewaongoza polisi kwa ajili ya ukamataji.
Ilivyokuwa
Taarifa za kuolewa kwa binti huyo zilitolewa na wasiri kwa uongozi wa kata na Jeshi la Polisi walioweka mtego wa kuwakamata watoto hao waliokuwa wanaozeshwa.
Uozeshaji wa watoto unaendelea wilayani humo, licha ya Shirika la Action Aid kuliwezesha Jukwaa la Wanawake Wilaya ya Chamwino (Juwacha) kuwasaidia watoto wa kike kuendelea na masomo.
Mwananchi lilifika kijijini hapo na kushuhudia shehere kubwa ikiendelea, huku wazazi wa pande zote mbili wakishiriki.
Kwa kawaida ya kabila la Wagogo, ndoa ya kimila hufanyika jioni na mwanamke anapochukuliwa haitakiwi aondoke mchana wa jua kali, utaratibu uliozingatiwa katika tukio la juzi.
Baada ya waoaji kufika, taratibu ziliendelea kama kawaida kwa binti kuogeshwa ndani kisha kutolewa nje ambako aliunganishwa na mumewe kwa ajili ya kupewa nasaha (malajilizo) ambayo hutolewa na pande zote.
Binti alisimama na kuwatambulisha baadhi ya ndugu zake kwa uchache kisha kijana alipewa nafasi ya kufanya hivyo kwa ndugu zake, ingawa hakujiamini hivyo akampa nafasi hiyo kaka yake amsaidie kufanya utambulisho huo.
Kwenye nasaha zake, mama mdogo wa binti huyo aliyejitambulisha kwa jina la mama Judi, alimtaka mtoto huyo kwenda kuitunza ndoa yake na kwamba moja ya ujasiri wa kuolewa ni kuvumilia magumu bila kutoa taarifa nyumbani.
Kaka wa binti huyo aliyejitambulishwa kama Eliud Mhanjilwa, alimtaka msichana huyo kutambua katika ukoo wao hawana desturi ya kuvunja ndoa, hivyo hatakiwi kurudi nyumbani na kwamba kama atakuwa na wazo la kurudi akatafute mahari ya kumrudishia mumewe.
“Ase kwetu hono mwana we chidala yatolwa hodu katolwa, sichigomola sawo za munhu ase hamba hadodo, hono mwileche bite kalondole kunji ugomole gwegwe ninga hetu sikokwinjila (kwetu binti akiolewa ni ameolewa, huwa hatuna utamaduni wa kurudisha mahari hata kidogo na ikitokea mkaachana nenda katafute kwingine mahari za kurudisha kwa mumeo lakini kwetu hutoingia),” alisema Mhanjilwa.
Ndoa za utotoni Chamwino
Wilaya ya Chamwino inatajwa kuwa na matukio mengi ya ndoa na mimba za utotoni sambamba na ukeketaji.
Mwenyekiti wa Juwacha, Janeth Nyamayahasi alisema wanakabiliana na mambo mengi katika kuwasaidia wasichana kufikia ndoto zao maishani.
Nyamayahasi alisema kupitia jukwaa lao ambalo linawezeshwa na Action Aid, wamefanikiwa kuwapa elimu wanawake na hayo ndiyo matunda yake, kwani kila sehemu wamepeleka elimu hivyo kuwa na mashujaa wanaosaidia kuliokoa kundi la watoto wa kike.
Juzi, polisi wanne walienda eneo la tukio na kunyoosha moja kwa moja mpaka mahali walipokaa maharusi na kuwashika mikono kisha kuwafunga pingu na kuondoka nao pamoja na wazazi wao, lakini hawakutaka kuzungumza, hali iliyowaacha wageni waalikwa wakitawanyika.
Watu watano walikamatwa wakiwamo watoto hao, baba na mama wa bibi harusi na baba mzazi wa bwana harusi