MHADHIRI wa uchumi kutoka Chuo kikuu caha Dar Es Salaam, Profesa Humphrey Moshi, amemtaka waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba pamoja na timu yake inayohusika na masuala ya kodi kubadilika na kuwa wabunifu badala ya kutegemea vyanzo rahisi rahisi vya kikodi. Anaripoti Erick Mbawala TURADRCo … (endelea).
Hatua hiyo imekuja baada ya Sheria ya Tozo ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2022, kuanza kutumika hivi karibuni na kusababisha tozo kuanza kukatwa kwenye miamala ya kifedha kupitia benki hali inayotajwa kuongeza makali ya ugumu wa maisha kwa watumiaji wa huduma husika.
Dk. Nchemba kupitia gazeti la Serikali No.478 lililochapishwa tarehe 1 Julai, mwaka huu, alitangaza kuanza utekelezaji wa kodi ya miamala ya fedha kupitia benki.
Aidha, akizungumzia hatua hiyo, Prof. Moshi amesema licha ya kwamba awali hapakuwa na matumizi makubwa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama ilivyo sasa hali inayolazimu tozo kuwa na wigo mpana, bado katika masuala ya uchumi watoza tozo nao wanatakiwa kubadilika na kuwa wabunifu.
Akizungumza na MwanaHalisi Online leo tarehe 21 Agosti, 2022, Prof. Moshi amesema ni dhahiri kuwa mfumo wa uchumi wa nchi umebadilika hivyo tozo nazo zinaendelea kubadilika kufuatana na mabadiliko ya mifumo ya uchumi, jambo ambalo ni kawaida mahali popote duniani.
Amesema kutokana na hali hiyo baadhi ya tozo zilizokuwa kwenye sekta ya TEHAMA zilikuwa sahihi lakini hizi zinazobambikwa kwenye miala ya simu na benki sasa zinaleta mvurugano kwani zimekuwa nyingi mpaka zinakuwa kero na watu wanajaribu kuzikwepa.
Amesema suala la kodi lazima iwaguse watu wote wanaofaidika na huduma muhimu kama barabara, afya na miundombinu mingine, lakini ubunifu unahitajika ili kutowaumiza watu wa kada ya chini kama vile mama ntilie, waendesha pikipiki na bajaji.
Ametoa mfano kuwa kuna baadhi ya sekta ambazo bado ukusanyaji wa kodi hauridhishi hususani katika sekta ya uuzaji wa magari.
Amesema uuzaji wa magari katika siku za karibuni umekuwa holela kila baada ya mtaa kuna yadi ya magari au kuna maegesho ya kuuza magari.
Vivyo hivyo katika maeneo ya vituo vya mafuta ambako kote hakuna ukusanyaji wa kodi jambo ambalo linaweza kudhaniwa ni mojawapo ya eneo la utakatishaji fedha.
“Ukiangalia kwa makini hata wafanyabiashara hao wa magari wana watu wengi wanafanya nao biashara lakini hawana mashine za risiti za EFD, hivyo lazima kuwa wabunifu, waache kuangalia mahali pamoja tu na kuwalimbikizia wachache,.
“Vifaa vya EFD visambazwe na kuwe na usawa kwenye malipo ambapo mwenye uwezo mdogo alipe kulingana na uwezo wake tofauti na mwenye uwezo mkubwa,” amesema.
Pia amesema inapaswa kuangalia namna ya kutoza kodi Sekta zisizo rasmi ambazo zinachukua takribani asilimia 64, ili nazo zichangie katika maendeleo ya Taifa.
“Lazima Mamlaka ya mawasiliano (TCRA) wahamasishe watu ili waelewe hizo fedha za tozo zinatumika katika kufanya mambo gani ya kimaendeleo.
“Mfano kosa kubwa ambalo lilifanywa na serikali ni katika suala la kuongea gharama za mafuta, kosa lingine kubwa zaidi ni kukosa washauri wenye upeo mkubwa wa mawazo au wanatumia washauri wenye umri mdogo na ufinyu wa mawazo” amesema na kuongeza kuwa;
“Unapofanya mafuta ya petrol yawe ghali kuliko dizeli wakati zaidi ya asilimia 95 ya magari ya biashara kama mabasi pamoja na malori hutumia petroli, hapo ni kurudisha nyuma pato la serikali na makosa ya namna hiyo ndo yanakwamisha uchumi, hivyo wajaribu kupanua wigo wa kiuchumi”.