RAIS Mteule William Ruto Apata Pigo Kesi ikianza




RAIS Mteule William Ruto amepata pigo baada ya Mahakama ya Upeo kutupilia mbalimbali mengi ya maombi yake huku kesi ya kupinga ushindi wake ikiwa imeanza kusikilizwa leo Jumatano.

Mahakama hiyo ilikataa ombi la Dkt Ruto kutaka Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kizuiwe kushirikishwa katika kesi ya kupinga ushindi wake.

Mawakili wa Dkt Ruto walitaka chama cha LSK kisishirikishwe kwenye kesi hiyo kutokana na kigezo kwamba mwaniaji mwenza wa Azimio, Martha Karua, ambaye ni mmoja wa walalamishi, ni mwanachama na kiongozi wake wa zamani wa LSK.

Chama cha LSK kilituma maombi ya kushirikishwa katika kesi hiyo ambapo mwaniaji wa urais wa Azimio Raila Odinga anapinga ushindi wa Dkt Ruto, kikisema kuwa kina tajriba na utaalamu katika masuala ya kisheria na kinaweza kusaidia mahakama kufanya uamuzi mwafaka.


Lakini Dkt Ruto alipinga akisema kuwa chama hicho huenda kikapendelea upande wa Bw Odinga.

Jaji Mkuu Martha Koome na wenzake Philomena Mwilu, William Ouko, Mohammed Ibrahim, Dkt Smokin Wanjala, Njoki Ndungu na Isaac Lenaola pia walikataa ombi la Dkt Ruto kutaka nyaraka za viapo za kibinafsi na ushahidi uliowasilishwa na makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zitupiliwe mbali.

Makamishna wa IEBC Juliana Cherera, Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya wamewasilisha maombi na ushahidi wa kupinga matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wao Wafula Chebukati mnamo Agosti 15, 2022, ambapo Dkt Ruto alitangazwa mshindi.


Makamishna wengine Bw Chebukati, Boya Molu na Abdi Guliye wanaunga mkono ushindi wa Dkt Ruto.

Mahakama ya Upeo pia ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto iliyotaka kesi ya Bw Odinga itupiliwe mbali.

Bw Kuria na Mbunge wa Mbeere Kusini Geofrey King’ang’i walitaka Mahakama ya Upeo itupilie mbali kesi ya Bw Odinga kwa madai kwamba alisababisha vurugu katika ukumbi wa Bomas muda mfupi kabla ya Dkt Ruto kutangazwa mshindi.

USHAHIDI WA GITHONGO

Juhudi za Dkt Ruto kutaka kuzima ushahidi uliotolewa na mwanaharakati John Githongo pia ziligonga mwamba baada mahakama kuuruhusu kwenye kesi.


Bw Githongo katika ushahidi wake anadai kuwa kambi ya Dkt Ruto ilifadhili wadukuzi kuvuruga fomu za matokeo katika sava za IEBC.

Dkt Ruto alitaka ushahidi wa Bw Githongo kutupiliwa mbali kutokana na kigezo kwamba ulikuwa ni uvumi.

Lakini majaji walisema kuwa ilikuwa mapema kutupa ushahidi huo.

Chama cha Farmers ambacho ni moja ya vyama vilivyo ndani ya muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Dkt Ruto nacho kilizuiliwa kujiunga na kesi.


Wakili wa Dkt Ruto, Fred Ngatia alilalamika mahakamani kuhusu idadi ndogo ya mawakili wa kutetea ushindi wa Rais Mteule ambao mahakama imeruhusu kumwakilisha.

Bw Ngatia pia alilalamikia masaa ‘machache’ yaliyotengewa upande wa kutetea ushindi wa Dkt Ruto.

“Mawakili 16 wa upande wa unaopinga ushindi wa Dkt Ruto wameruhusiwa kuingia ndani ya korti lakini upande wetu ni mawakili wanne pekee,” Bw Ngatia alilalamika kortini jana Jumanne.

Wakili Ngatia pia aliomba upande wa utetezi kuongezewa saa moja ili kuweza kujibu madai yote yanayotolewa na upande wa walalamishi.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Jaji Mkuu Koome, upande wa wanaotaka ushindi wa Dkt Ruto kubatilishwa umetengewa jumla ya masaa saba ya kuzungumza kortini ilhali upande wa utetezi ukipewa masaa sita.


Tume ya IEBC na Dkt Ruto wamepwa jumla ya masaa sita kuthibitishia korti kwamba uchaguzi ulikuwa huru na haki.

Upande wa walalmishi unaojumuisha Bw Odinga na walalamishi wengine sita pamoja na makamishna wanne wanaoongozwa na Bi Cherera wametengewa jumla ya muda wa saa saba.

Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki ambaye tayari amesema kuwa hatapinga kesi ya Bw Odinga amepewa dakika 30 kuwasilisha kesi kortini.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mkuu wa Sheria kujitenga na IEBC katika kesi ya kupinga matokeo ya urais tangu 2013.

Wamatangi azuru afisi mbalimbali za kaunti akiahidi...
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad