RAIS Samia Suluhu Hassan amesema hivi karibuni wakuu wa wilaya wataanza kutimuana tena kwa ajili ya usimamizi wa ujenzi wa madarasa 8000 ya shule za sekondari ili kujiandaa na mapokezi ya wanafunzi wapya wa kidato cha kwama mwaka 2023.
Pia amesema mkoa wa Mbeya umepata ngekewa kwa kupatiwa miradi 50 ya maji ikiwa ni utekelezaji wa ahadi walizoahidi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 6 Agosti, 2022 wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Chalangwa iliyopo wilayani Chunya mkoani humo ambapo amesimama kuwasalimia wakazi wa kata hiyo.
Rais Samia ambaye jana ameanza ziara mkoani humo, amesema, “Kuhusu ujenzi wa madarasa hivi karibuni tutaanza kutimuana tena, halmashauri ma-DC kaeni vizuri… mwakani tutahitaji madarasa 8000 ya sekondari kwa Tanzania nzima,” amesema.
Kuhusu umeme vijijini amesema wataensdelea kupeleka umeme vijijini, kujenga vituo vya afya na ujenzi wa barabara kama walivyoahidi.
“Ujenzi wa barabara tunaendelea nao, kama mnavyojua ujenzi wa barabara ni gharama kubwa mno, ni sawa na vituo vya afya 10 ndio kilomita moja ya barabara, lakini tutaendelea nao na tutajenga kama tulivyoahidi,” amesema.
Aidha, amewaomba wananchi wa mkoa huo kufanya kazi na kulima kwa bidi ili wapate fedha za kujiletea maendeleo.
“Pia niwaombe mshiriki zoezi la sense… tunataka kujuana tupo wangapi, madhumu ya kutaka kujua hesabu zote hizo ni kupanga mipango yetu ya maendeleo, tunapopanga fedha iende wapi, tujue tunapanga kwa watu wangapi,” amesema.
Awali waziri wa ujenzi na uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema wizara hiyo imetenga kiasi cha Sh milioni 200 kwa ajili ya kufunga taa 65 za barabara katika wilaya ya Chunya.