MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema hakuwahi kuwaza kuongoza mkoa huo ambao ni makao makuu ya nchi.
Senyamule alisema hayo jana mjini Dodoma wakati aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo, Anthony Mtaka akimkabidhi ofisi. Kwa sasa Mtaka ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe.
"Sikuwahi kuwaza kuhamia Dodoma hata majina ya uteuzi yalipotoka nikawa naangalia mara mbilimbili nasema ni mimi kweli au nimekosea, nikajiuliza ni mimi kweli naenda Dodoma, nikaanza kupata simu za salamu na hongera unaenda makao makuu ya nchi zile salamu zikanipa tafakuri," alisema.
Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na akasema alikuwa akimfahamu Mtaka kama mtu mwenye mikakati ya kutosha kutokana na kufanya kazi kubwa Simiyu na hata Dodoma.
Kwa mujibu wa Senyamule, kitu ambacho alitamani Mtaka akimalizie ni kuwahamishia wafanyabiashara kwenye soko jipya la Machinga.
"Vipaumbele vyangu vitategemea sura ya Dodoma kama makao makuu ya nchi na hata nje ya mji kuna mengi ya kufanya ili maeneo hayo yawe na sura ya makao makuu ya nchi,” alisema.
Senyamule alitaja vipaumbele vingine kuwa ni kwenye migogoro ya ardhi, utunzaji mazingira na uchumi.
Aliomba wananchi wa Dodoma wampokee kwa namna alivyo ingawa anafahamu wata-mmiss sana Mtaka.
"Wananchi wa Dodoma hawawezi kuwa yatima, wangojee mabadiliko naitwa Rosemary, yale mazuri aliyoyaanzisha Mtaka nitayaendeleza, nitafanya kwa ajili ya wananchi," alisema.
Mtaka alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kumuamini na kumteua kuwa Mkuu Mkoa wa Njombe na akasema kwa umri wake anafurahi kufanya kazi maeneo tofauti.
Alisema kwa mara ya kwanza aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya mwaka 2012 akiwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro pia amewahi kufanya kazi Wilaya ya Hai, baadae aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kisha Dodoma na sasa Njombe.
“Marais watatu waliniamini na kuniteua Rais Mstaafu Jakaya Kikwete aliniteua kuwa DC, Hayati John Magufuli aliniteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na Rais Samia Suluhu Hassan ameniteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe," alisema.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk Fatma Mganga alisema watatoa ushirikiano kwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Dodoma.