Dar es Salaam. Agosti 15, 2022 ni siku ambayo haitasahaulika kwa William Ruto, familia yake, wafuasi na mashabiki waliokuwa wakimuunga mkono katika harakati ya kusaka urais wa Kenya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2022.
Siku hiyo ndiyo aliyotangazwa kuwa Rais mteule wa Kenya, kazi hiyo ilifanywa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, Wafula Chebukati ambaye kabla ya kufanya hivyo kulitokea vurugu kwenye ukumbi wa Bomas, ambao ulikuwa ukitumika kutangazia matokeo na kuhakiki kura za urais kutoka vituoni.
Ahadi ya Ruto
Mara baada ya kutangazwa mshindi, Ruto alikutana na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa kutangazia matokeo hayo wa Bomas, akisisitiza kuwa hataua upinzani, bali atachochea demokrasia ya vyama vingi.
Alisema bila upinzani makini Serikali haiwezi kuwajibika ipasavyo, atafanya kama Rais Uhuru Kenyatta, aliyeamua kushirikiana na mpinzani wake, Raila Odinga.
“Sijawahi kuamini kwenye hadithi za maridhiano na upinzani (handshakes) kwa sababu naamini katika demokrasia, kwa sababu ukiwa na Serikali ambayo haina upinzani unaitengeneza Serikali isiyowajibika kama kitu tulichokishuhudia miaka minne iliyopita,” alisema Ruto.
“Badala ya Serikali kukosolewa na wapinzani sasa wapinzani wanakuwa wanaunga mkono masuala ya kiserikali, kitu ambacho sitakihitaji kwenye Serikali yangu,” aliongeza.
Abomoa upinzani
Agosti 17, 2022 Ruto alikutana na viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya muungano wao wa Kenya Kwanza na alitangaza kuwapokea wabunge 10 wasio na chama (wagombea binafsi) kwenye muungano wao wa Kenya Kwanza.
“Tuna wabunge 163 kwenye muungano wetu wa Kenya Kwanza, lakini 140 wa chama cha UDA, wakiwemo wabunge wa viti maalumu, maseneta 24 na tumewapokea wabunge wengine 10 wa kujitegemea wamejiunga na timu yetu, tuna imani kwamba wengine wawili waliosalia watakuja upande wetu,” alisema.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2022, wagombea binafsi 12 walishinda ubunge na kati yao 10 ndio walitangazwa kujiunga na Kenya Kwanza na kusalia wabunge wawili binafsi wakiwa hawana chama.
Bila kujali kuhusu upinzani ambao siku mbili nyuma aliahidi kuuhitaji kwenye uongozi wake kwa ajili ya uwajibikaji wa Serikali, Ruto hadharani akaahidi tena wengine (wabunge) wataendelea kuhamia Kenya Kwanza, hasa wale wawili waliosalia ambao hawana vyama.
Hapa unaweza kusema kuwa, Ruto ameonyesha kuwa na ndimi mbili kuhusu jambo moja, wakati anasema anahitaji upinzani wenye nguvu kwa ajili ya kukosoa, lakini wakati huohuo anaubomoa upinzani kwa kuzoa wabunge kutoka sehemu nyingine ili wawe upande wake na wampitishie mambo yake kwenye nyumba ya maamuzi (Bunge).
Hili linaweza kuwa sio jambo la kushangaza sana kwa wanasiasa kuwa na tabia kama ya Ruto, hapa ananikumbusha kitabu cha mwandishi mahiri wa habari za siasa na diplomasia duniani, Paul Vallely kinachoitwa ‘Two faces and a forked tongue: The key components of a political toolkit’ ambacho ndani yake kinaeleza kuwa na sura mbili na ndimi mbili kwa mwanasiasa ni moja kati ya zana muhimu kwenye kutimiza majukumu yake.
Kwanini Ruto anafanya haya?
Mosi, anatafuta kulimiliki Bunge, ikiwemo kumpata spika kutokea upande wake na pili anataka kuonyesha kuwa awamu iliyopita ya uongozi chini ya Rais Uhuru Kenyatta ilifanya vibaya.
Kuhusu kulimiliki Bunge na kumpata Spika wa Bunge kutoka upande wake, kanuni za Bunge la Kenya zinasema kuwa ili maamuzi yapitishwe na Bunge hilo lenye wabunge 349, ni lazima theluthi mbili iridhie, huku kiwango hicho kikiwa sawa na idadi ya wabunge 233 ambao Kenya Kwanza haijafikia.
Kenya Kwanza ina wabunge 164, wanahitaji wabunge 69 zaidi ili waweze kupitisha baadhi ya mambo yao bungeni, zikiwemo sheria, huku wapinzani wao, Azimio la Umoja wakiwa na wabunge 167. Kwa hiyo Ruto anavuta wabunge wengi upande wake ili mambo yake yapite kwenye nyumba hiyo ya maamuzi, lakini pia ili mgombea wao kiti cha uspika ashinde.
Vita na Azimio la Umoja
Ruto hajaishia kwa wabunge wasio na chama tu, inasemekana sasa hivi anaingia hadi kwa washindi wa ubunge kwa tiketi ya Azimio la Umoja ambao ni wapinzani wao wakubwa, jambo ambalo limeibua taharuki kwa viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja waliotishia kuwavua uanachama na ubunge endapo wakihamia kwa mahasimu wao wa Kenya Kwanza.
Pia, Ruto anaingia kwenye mtego wa kuonekana ana ndimi mbili au kigeugeu, kwa sababu anajaribu kuonyesha utawala uliopita haukuwa sawa kwenye baadhi ya mambo, kwa bahati nzuri au mbaya utawala uliopita alikuwa miongoni mwao kabla ya kugombana na Rais wake, Uhuru Kenyatta na kuwa maadui wa kisiasa.
Kenyatta aliingia kwenye ugomvi na Ruto baada ya kumshutumu kufanya siasa na michakato ya kuwa Rais kabla ya muda, huku pia ikikumbukwa Ruto alipinga vikali mpango wa marekebisho ya katiba ya nchi hiyo maarufu kama BBI, uliokuwa unapendekezwa na Kenyatta ambao ulilenga kuongeza baadhi ya vyeo kwenye serikali kuu, kama vile uwaziri mkuu.
Azimio waja juu
Msemaji wa kampeni za Raila Odinga, Profesa Makau Mutua, anasema kinachofanywa na Ruto ni ukiukaji wa sheria na dhamira ya kuirudisha nchi enzi za utawala wa KANU, ambako kulikuwa na rushwa ya kisiasa.
“Ruto asiruhusiwe kuirejesha nchi yetu miaka ya nyuma ya utawala wa kidikteta chini ya KANU, napaswa akomeshe utaratibu wa kujihusisha na rushwa za kisiasa, nchi hii ni ya vyama vingi, atambue hilo na aache demokrasia itamalaki badala ya kuwarubuni wabunge wetu walioshinda na wale wasio na vyama,” alisema Mutua.