SAKATA la kipa Metacha Mnata kusaini Singida Big Stars wakati akiwa na mkataba wa mwaka mmoja na Polisi Tanzania, limefika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Charles Mkumbo ameweka wazi kushitaki TFF, kuhusiana na hilo, huku akishangazwa na maamuzi ya kipa huyo kusaini SBS akijua ni makosa kisheria.
"Tulishangaa kuona Metacha amesaini SBS akijua ana mkataba wa mwaka mmoja na sisi, tumeamua kuzingatia sheria na kanuni za soka tumepeleka jambo hilo TFF," amesema na kuoneza;
"Tunasubiri majibu ya TFF kuhusiana na Metacha, maana sisi tuna vielelezo vyote vinavyoonyesha ni mchezaji wetu."
Mtendaji mkuu wa SBS, Mhibu Kanu aliwahi kukaririwa kwamba hawakujua kama mchezaji ana mkataba na Polisi Tanzania, lakini ni jambo ambalo walihitaji kukaa mezani ili kulimaliza.
"Ni jambo la kukaa mezani, kwani mchezaji wakati anasaini aliulizwa na akasema hana mkataba," amesema.