Dodoma. Licha ya changamoto za uandikishaji Sensa ya Watu na Makazi kuibuka, hususan vishikwambi vinavyotumiwa na makarani na malalamiko ya wananchi kuhusu kucheleweshwa na wengine kusubiri kuhesabiwa kwa muda mrefu katika maeneo mbalimbali nchini, uandikishaji umevuka lengo hadi kufikia asilimia 17.1.
Changamoto nyingine ambazo zimeripotiwa maeneo mbalimbali ni baadhi ya makarani kushindwa kutumia kwa ufasaha vishikwambi, ukosefu wa umeme na mtandao wa intaneti unaosababisha shughuli hiyo kwenda taratibu.
Ni sensa ambayo imeshuhudia mwamko mkubwa kwa wananchi kuwa na shauku ya kuhesabiwa, lakini wingi wa maswali na teknolojia inayotumika vimesababisha kwenda kwa kusuasua, jambo linalozidisha wasiwasi kwa wananchi kama wote watafikiwa kwa wakati.
Jana, Kamishna wa Sensa na Makazi, Anne Makinda alitoa tathimini ya siku moja ya kwanza ya kazi hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akisema lengo lilikuwa kuandikisha kwa asilimia 15 lakini wameandikisha asilimia 17.1.
Alisema sensa hiyo iliyoanza juzi inakwenda vizuri, kwani hadi jana asubuhi taarifa zinaonyesha asilimia 17.13 ya kaya zilizopo nchini zimerekodiwa katika kituo cha kuchakata sensa cha Dodoma.
Alisema lengo kwa siku ya kwanza lilikuwa kufikia asilimia 15.0 ya kaya, lakini wamevuka hadi asilimia 17.13, akisema hayo ni mafanikio makubwa katika mchakato huo ulioingia siku ya tatu leo.
Makinda, aliyewahi kuwa Spika wa Bunge, alisema anafahamu kuwa kila mwananchi angependa kuhesabiwa juzi kwa sababu ilikuwa ni siku ya mapumziko, lakini haikuwa rahisi.
Kutokana na hali hiyo, Makinda amewaomba wananchi wa kaya ambazo makarani hawajapita kuwa na subira katika kipindi cha siku sita zilizobaki. Alibainisha kuwa taarifa za wanakaya zinazohitajika ni zile waliolala eneo husika usiku wa kuamkia Agosti 23.
Alisema karani atapita katika kaya kuweka miadi na mkuu wa kaya na kuacha fomu maalumu ambayo atajaza taarifa muhimu za watu wote waliolala katika kaya yake usiku wa kuamkia Agosti 23.
“Fomu hii imeainisha taarifa hizo, hivyo tunawasihi wakuu wa kaya kujaza fomu hizo ili kurahisisha ukusanyaji wa taarifa wakati karani wa sensa atakapofika kufanya mahojiano. Waratibu wa sensa wa mikoa na wilaya wahakikishe fomu hizo zinasambazwa katika kaya ili kuharakisha mchakato huu,” alisema Makinda.
Kamishna huyo, aliwataka makarani kufika kwa wakati katika makazi ya watu, akisema sensa inafanyika asubuhi mkuu wa kaya hajaondoka kwenda kazini, halikadhalika muda wa jioni baada ya mkuu wa kaya kurejea kutoka kazini.
Makinda aliwataka waratibu wa sensa wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanaandaa utaratibu wa kuwa na namba rasmi ya simu itakayotumiwa na wananchi kupiga endapo hawajahesabiwa kabla ya Agosti 29, ili utaratibu maalumu uwekwe wa kuwafikia.
Kuhusu suala la viongozi wa mitaa na vitongoji kuongozana na makarani wa sensa, Makinda alisisitiza kila kiongozi mmoja anapaswa kumuongoza karani mmoja wa Sensa na malipo yao yameandaliwa.
“Uzoefu tulioupata Agosti 23 kuna baadhi ya viongozi hao wanalazimisha kuongoza makarani zaidi ya mmoja, jambo ambalo linachelewesha mchakato huu,” alisema Makinda.
Tatizo la mipaka
Kamisaa huyo alisema Sensa ya Watu na Makazi haina mamlaka ya kurekebisha mipaka, akisema mchakato huo unahusisha maeneo ya kuhesabia watu yaliyotengwa maalumu kwa kazi hiyo.
“Nawaomba wananchi walio katika maeneo kama hayo wawape ushirikiano makarani wa sensa ili kutekeleza majukumu yao, huku mamlaka husika zikishughulikia matatizo hayo ya mipaka,” alisema Makinda.
Suala hilo la mipaka limeibuka kwa wakazi wa Zingiziwa ambako kulikuwa na ubishani ambapo Diwani wa eneo hilo, Maige Maganga, aliomba wananchi wasikatae kuhesabiwa kwa kuwa suala la sensa ni la kitaifa na sio la kimipaka.
Sambamba na hilo, aliwaahidi suala la mgogoro wa mipaka kati yao na Kisarawe, Mkoa wa Pwani kulishughulikia lipo palepale na kuwataka wapishe kwanza hili la sensa.
Kauli ya diwani inakuja baada ya baadhi ya wananchi Mtaa wa Ngobedi, hususan maeneo ya Nyota Njema, juzi kuwagomea makarani wa sensa kuwahesabu kwa kile walichoeleza wametokea Kisarawe wakati wao ni wakazi wa Ilala.
Kilio hicho kilifikishwa na viongozi wao katika serikali ya mtaa wa Ngobedi ambapo hata hivyo majadiliano kati yao na wasimamizi wa sensa katika eneo hilo hayakuweza kufikia muafaka.
Hata hivyo, kwa upande wake msimamizi wa sensa kituo cha Chanika, aliyefahamika kwa jina moja la Lameck, alisema walifika jana jioni eneo hilo na mtu wa takwimu na wameshashughulikia suala hilo.
Akifafanua suala la mipaka alisema wao wameyagawanya maeneo kulingana na NBS, ambapo mengine yanaingiliana na wilaya au mikoa mingine ambayo hiyo haina shida kwa kuwa nia ya Serikali ni kujua idadi ya watu iliyonayo.
Power benki kugawiwa
Mratibu wa Sensa Taifa, Seif Kuchengo alisema maeneo yenye changamoto ya umeme hasa vijijini, yatapelekewa majenereta ili kusaidia makarani kuchaji vishikwambi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, alisema pia makarani watagawiwa vifaa vya kuchajia ‘power bank’ vishikwambi vyao kwa waliopo mbali na maeneo wanayoweza kupata umeme.
Kuchengo alisema makarani wamepatiwa mafunzo yatakayowawezesha kutumia simu kama mbadala pale vishikwambi vitakapopata changamoto.
Kuhusu makarani waliopoteza au kuibiwa vishikwambi, alisema uchunguzi maalumu utafanyika na utaratibu wa kuwapatia vishikwambi vingine utafuatwa.
Umeme ni tatizo
Jana, mmoja wa makarani mkoani Dodoma ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema changamoto ambayo wamekutana nayo ni vishikwambi kuisha chaji wakati wakikusanya taarifa.
Alisema vishikwambi hivyo vinakaa na chaji kwa saa nane hadi 10 na hivyo pindi vinapoisha chaji wanakutana na wakati mgumu kuwaelekeza wanaowahesabu kwamba vimeisha chaji.
Pia, alisema changamoto hiyo imekuwa ikiwapa wakati mgumu kwa sababu inawabidi kwenda katika nyumba za wahesabiwa ama kurudi kwenye ofisi za watendaji wa kata ambako ndiko kuna umeme.
“Mfano mimi kiliisha chaji kikazima, ikabidi nirudi katika ofisi za kata ya Viwandani ili niweze kuchajisha tena kwa nusu saa mpaka saa zima, ukirudi kule mtu anakuona wewe kama vile ni mzembe,” alisema
Alisema changamoto nyingine ni kusubiriwa kwa hamu na wanaohesabiwa huku baadhi wakihoji ni kwa nini wanachelewa.
Anachokieleza karani huyo wa Dodoma ni sawa na kilichotokea Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ambapo umeme umesababisha baadhi ya maeneo kufanyika kwa kasi ndogo.
Mratibu wa Sensa wa Wilaya ya Simanjiro, Linus Mboya aliwatoa hofu wananchi akisema wote watafikiwa, kwani watahesabiwa kwa muda wa siku saba.
“Wana Simanjiro wasihofu watahesabiwa wote, kwani baadhi ya vishikwambi havina power bank na maeneo mengine hakuna umeme wa kuchaji, ndiyo sababu kunakuwa na kasi ndogo ila watafikiwa wote,” alisema Mboya.
Nako Mkoa wa Tanga, Jeshi la Polisi mkaoni Tanga limewaachilia makarani watatu katika wilaya za Handeni na Korogwe waliokuwa wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano kutokana na kupoteza vishikwambi.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Sofia Jongo alisema ni kweli kuna makarani wawili wilaya ya Handeni na mmoja Korogwe walipoteza vishikwambi vyao ila vimepatikana na wanaendelea na kazi.
“Kuna makarani walipoteza vishkwambi, ila kwa sababu vina kifaa maalumu vya kujulikana vilipo tulivipata na kuwarudishia na sasa wanaendelea na kazi yao ya sensa, ila matukio haya yalitokea nyuma kabla ya kuanza shughuli ya kuanza kuhesabu watu na sio baada ya kuanza sensa,” alisema Jongo.
Hali kama hiyo imejitokeza katika Kijiji cha Tondoroni kata ya Kiluvya, Wilaya ya Kisarawe mkoani wa Pwani, ambapo wananchi wa kijiji hicho walitoa kilio chao kwa Rais Samia Suluhu Hassan, wakieleza wameshindwa kuhesabiwa kwa madai kijiji chao hakipo kwenye ramani ya sensa ilhali kimesajiliwa kisheria.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Nickson Simon alifika eneo hilo na kuzungumza na wananchi na baada ya kumuelewa walikubali kuhesabiwa.
Mtandao shida
Wilayani Musoma, Mkoa wa Mara, ukosefu wa mtandao wa intaneti katika baadhi ya maeneo wilaya ya Musoma makarani wa sensa wanalazimika kuchukua taarifa za watu na makazi kisha kuzijaza baadaye wanapokuwa katika eneo lenye mtandao.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule, akizungumza na gazeti hili ofisini alisema “kuna baadhi ya maeneo hasa kule vijijini ambapo hakuna mtandao kabisa, kwa hiyo makarani wanachukua taarifa na kuzitunza wakifika kwenye mtandao wanazituma moja kwa moja NBS.”
Alisema kutokana na changamoto ya mtandao huo katika baadhi ya maeneo, makarani hao walifundishwa namna ya kufanya wanapokutana na changamoto hiyo hivyo ukosefu huo wa mtandao haujaathiri shughuli hiyo iliyoanza jana nchini kote.
Aliwaondoa hofu wakazi wa wilaya hiyo ambao hadi sasa hawajahesabiwa kuwa lazima watahesabiwa kabla ya siku saba za sensa kuisha.
Mkoani Mtwara, baadhi ya wananchi wa manispaa ya Mtwara Mikindani walisema kasi ndogo ya makarani wa sensa inatokana na kutokuwa na ujuzi wa matumizi ya kishikwambi.
Ally Juma, mkazi wa Magomeni alisema Serikali ilipaswa kuwaandaa kwa muda mrefu kwa kuwa wengine hawana ujuzi wa matumizi ya hicho kifaa.
Alisema matumizi ya kifaa hicho yanapaswa kutumiwa na mtu mzoefu ili kwenda kwa kasi kukamilisha ukusanyaji wa taarifa kwa wakati.
“Mfano karani aliyekuja kwangu yaani hadi huruma, anavyodonoa donoa yaani anakaa na wewe muda mrefu hadi unajiuliza ataweza kufanikisha lengo la Serikali la kuhesabu kwa siku saba, kwa nini hawakuchukuliwa wazoefu wapo?” alihoji Ally.
Wenye ulemavu Dar
Jijini Dar es Salaam, Chama cha Wenye Ulemavu Waendesha Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam (Uwabada) kimesema, ili kuwarahisia kazi makarani wa sensa, wapo tayari kujumuika eneo moja ili wahesabiwe.
Kilisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kila mwanachama wao anapata haki ya kuhesabiwa, kwani wapo baadhi ya wanachama wao wameanza kukata tamaa baada ya juzi siku ya ufunguzi wa sensa kitaifa kuwasubiri makarani nyumbani bila mafanikio.
Mwenyekiti wa Uwabada, Paul Masamaki akizungumza na gazeti hili alisema wakati wa ufunguzi wa sensa aliwahimiza wanachama wake kubaki nyumbani ili wahesabiwe, lakini hakuna yeyote miongoni mwao aliyefikiwa.
“Tuna vituo vitatu vikubwa, Feri, Congo na Mnazi Mmoja, wanachama hawa wote wanaweza kujumuika eneo moja, tukiletewa karani na tukahesabiwa kwa urahisi, njia hii ni rahisi kwa sababu wote tunapatikana eneo moja, tuliona wengi waliofikiwa ni viongozi,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Uwabada, Jackline John alisema amekuwa akipokea simu nyingi kutoka kwa wanachama wake walioonyesha wasiwasi wa kukosa nafasi ya kuhesabiwa.
“Kabla ya sensa nilizunguka kuwapa elimu, nilikuwa balozi wa kuwapa elimu ndio maana wakanipigia, ni muhimu kupitia umoja wetu sasa kwenye eneo hili tukaletewa karani ambaye atachukua taarifa zetu na sisi tutahamasishana kuwepo wote kwenye eneo moja,” alisema.
Kwa upande dereva bajaji, Mursin Issa, alisema makarani kuwafikia kulingana na makundi yao kutawasaidia kutoachwa nyuma, kwani wengine hawana wa kuwaachia taarifa zao.
Malipo ya makarani
Mtakwimu Mwandamizi wa NBS, Emilian Karugendo alisema kulikuwa na changamoto ya malipo kwa makarani wa sensa waliotakiwa kulipwa kwa siku 16, badala yake wamelipwa kwa siku 15.
“Tuliona taarifa mitandaoni na kilichotokea ni makosa ya kibindamu ambayo tumeshayafanyia kazi na makarani wote watalipwa fedha zao kwa mujibu wa mkataba,” alisema Karugendo.
Imeandaliwa na Ramadhan Hassan, Sharon Sauwa, Doreen Parkshard (Dodoma), Beldina Nyakeke (Musoma), Joseph Lyimo (Manyara), Florence Sanawa (Mtwara), Rajabu Athumani (Handeni), Baraka Loshilaa, Nasra Abdallah, Hadija Jumanne na Bakari Kiango (Dar)