Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha TLP, Augustino Mrema unatarajiwa kuzikwa Alhamisi Agosti 25 katika kijiji cha Kiraracha mkoani Kilimanjaro.
Maziko hayo yatatanguliwa na ibada ya mazishi siku ya Jumatano itakayofanyika katika kanisa Katoliki Parokia ya Salasala kabla ya kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Agosti 22, 2022 na mwanaye, Michael Mrema wakati akitoa ratiba ya msiba.
"Ibada ya mazishi siku ya Jumatano itaanza saa saba mchana kabla ya safari ya Kilalacha kuanza," amesema.
Mrema aliyefariki dunia jana Jumapili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam alikokuwa anapatiwa matibabu.
Katika uhai wake amewahi kushika nyadhifa mbalimbali Serikalini ikiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Pia enzi za uhai wake, mwanasiasa huyo aliwahi kuwa mgombea urais kupitia NCCR-Mageuzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 baada ya kujiunga na chama hicho akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mrema aliwahi kuwa Mbunge wa Vunjo kupitia TLP na hadi amefikwa na mauti alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.