Siku za Mwisho za Augustino Mrema




Aliyekuwa Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema
Dar es Salaam. Kabla ya kuhitimisha Safari ya miaka 77 dunia, mwanasiasa nguli nchini, Augustino Mrema aliyefariki juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alitaka amani, upendo vitawale nchini sambamba na mkewe, Doreen Kimbi, kuheshimiwa, kulisikilizwa na kutunzwa.

Kwa mujibu wa mjukuu wa mwanasiasa huyo, Leonard Mrema, babu yake alitoa wosia huo alipokuwa anapigania pumzi yake ya mwisho wakati wakimuguza (yeye na mke wa marehemu).

Akizungumza na Mwananchi, nyumbani kwa marehemu Salasala jijini hapa mara baada ya taarifa za kifo kusambaaa, mjukuu huyo alisema babu yake aliwataka ndugu zake wamuheshimu na kumsikiliza mkewe (Doreen) kwani ndiye atakuwa mbadala wake hivyo asitokee mtu wa kumyanyasa.
Leonard ambaye pia aliwahi kuwa dereva na msaidizi wa karibu wa Mrema, alisema juzi alipigiwa simu na bibi yake akimuambia kuwa babu yake anamuita hivyo aende hospitali.

Alisema kutokana na majukumu ya kazi kumbana alilazimika kwenda saa 4 usiku kuitikia wito na kumsikiliza babu yake ambaye alipenda kuongea naye muda wote.
Alisema katika mazungumzo yake mbali na kutaka amani na upendo utawale nchini pia alitaka mke wake aheshimiwe.
Alisema babu yake alitoa kauli hiyo kutokana na ukaribu na mapenzi aliyokuwa nayo kwa bibi yake ambaye ndiye alikuwa mtu wa karibu kabla ya umauti na wakati alipokuwa akiumwa alimsaidia na kuwa tumaini lake.
“Kwa kweli kuna wakati hospitali walikuwa wanakaa kama watoto kwa sababu hadi hospitalini kuna wakati alikuwa akimuita bibi (mkewe) na kumuomba ambembeleze, alikuwa akiishi kwa furaha na amani mida wote,” alisema Leondard.

Alisema katika saa nne alizokaa naye, babu yake aliomba kuogeshwa mara tatu huku akimueleza kuwa kufanya hivyo kunamfanya kujisikia amani na vizuri.
“Hata tulipokuwa tumekaa muda huo alikuwa amechangamka anaongea anakula hadi bibi akawa ananiambia mbona kachangamka sana, kuna wakati nilimuambia umekuwa na nuru akasema kweli nikamjibu ndiyo,” alisema.
Alisema ilipofika saa nane usiku aliaga ili huku babu yake akimtaka kesho (jana) saa 11 asubuhi awahi ili aweze kumsaidia bibi yake kumsafisha.


Tarifa za msiba

Leonard alisema ilipofika saa 10 alfajiri, bibi yake alimpigia simu na kumuomba awahi kwendahospitalini kwa sababu hali ya babu yake imebadilika na alipomuuliza imekuwaje alishindwa kujibu zaidi ya kulia.
“Ilinibidi niende haraka, nilipofika nilimkuta nje ya wodi, nikamuuliza imekuwaje akasema nenda kamuombee babu yako, nilipoingia nilikuta madaktari wamemzunguka nikazuiwa nikawaambia mimi ni mjukuu alinihitaji ila niliambiwa kusubiri.”
Alisema alisubiri kwa zaidi ya saa moja kabla ya kuambiwa taarifa za kifo chake.

Atakavyomkumbuka

Akiwa mtu mwenye uso wenye huzuni, alisema atamkumbuka Mrema kwa sababu alikuwa mtu aliyemuangalia katika mambo mengi na kujifunza vitu tofauti.
Leonard alisema mara zote alipokuwa akikaa na marehemu alikuwa akipenda amuelezee hali ya kiuchumi na kisiasa ilivyo nchini.
Alisema akiwa msaidizi wake na dereva kati ya mwaka 2017 na 2020, alikuwa akimsaidia mambo mengi ikiwemo kumuandalia hotuba mbalimbali hata alipotaka kuongea na waandishi wa habari.
“Hata nilipoajiriwa, alikuwa kama ana mkutano alinipigia simu kuwa naenda sehemu fulani kuonana n mtu fulani naomba niandalie hiki, kama ni speech (hotuba) au chochote nilimuandalia,” alieleza.
Alisema ilikuwa haipiti siku mbili babu yake hajampigia simu na mara zote alipokuwa kimya alimuuliza kwanini hamkumbuki.
“Zikipita siku mbili ananipigia ananiambia kwa nini hunipigii simu mimi babu yako. Ni mtu ambaye nilikuwa naye karibu sana, hata alipokuwa na dereva mwingine kuna wakati alinipigia akitaka mimi ndo nimpeleke kama niko na muda nilimpeleka,” alisema.


Alivyomsaidia kuacha ujambazi

Katika msiba huo, alikuwepo mwombolezaji, Martin Kimanga alisema Mrema alimsaidia kuacha ujambazi baada ya kusalimisha silaha zake mwaka 1990 wakati huo marehemu akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Martin alisema hakuna mtu mwingine aliyemshawishi kuacha kazi ya ujambazi bali ni Mrema.
“Nakumbuka mwaka 1990 Mrema alivyotangaza mtu yeyote anayetumia silaha bila ya kufuata sheria aiwasilishe kwake ndipo nilimfuata na kumkabidhi,” alisema Martin.
Alisema baada ya kumkabidhi alimuomba amsaidie mtaji wa biashara kwa sababu silaha aliyomkabidhi ndiyo chanzo pekee cha kumpatia kipato kwa ajili ya kufanya uhalifu.
Martin alisema marehemu baada ya kusikia hivyo aliamua kumpatia Sh300,000 kwa ajili ya mtaji wa biashara.
“Kweli nilivyopata fedha ile niliamua kununua roba la mitumba kwa ajili ya biashar”alisema

Alibainisha kuwa marehemu Mrema alimshauri pia aokoke ili asahau kabisa kazi ya ujambazi.
“Kweli nilivyoingia kwenye wokovu nimesahau kabisa masuala ya uhalifu namshukuru sana Mrema kwa kuacha shughuli hiyo isiyopendeza kwa jamii,” alisema Kimanga.

Nyumbani kwa marahemu

Mara baada ya kupata taarifa za msiba, Mwananchi lilifika nyumbani kwake na kukuta taratibu mbalimbali za msiba zikiendelea.

Ndugu na majirani kutoka sehemu tofauti walikuwa wakifika kutoa pole kwa wafiwa huku maandalizi mengine ya msiba yakiendelea kufanyika.

Vikao vilivyokutanisha wanandugu vilikuwa vikiendelea na hadi saa 12 jioni Mwananchi, lilipokuwa likiondoka katika eneo hilo bado wanandugu walikuwa wakiendekea na majadiliano na haikuelezwa mara moja ni lini na wapi maziko ya mwanasiasa huyo yatafanyike.

Wenzake wanavyomkumbuka

Mwanasiasa mkongwe, Getrude Mongella alisema Mrema ni mwanasiasa aliyedhibiti maovu wakati ambao wengine wasingeweza kusema kitu.

Alisema alifurahishwa zaidi na kiongozi huyo, pale ambapo wengine waliona aibu kukemea ukatili dhidi ya wanawake, yeye hakusita kwani alifanya hivyo hadharani.

Katika siasa za upinzani, alisema Mrema alizifanya kwa busara, aliheshimu taratibu sheria na watu wengine, sio kutukana kama wanavyofanywa na baadhi yao.


Naye Anna Abdallah, aliyemkumbuka Mrema kwa mtindo wake wa kusimamia anachokiamini na hilo lilijidhihirisha katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 alipoamua kumuunga mkono mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli.

Naye Thomas Ngawaiya, alisema wakati wote wakiwa pamoja Mrema alikerwa na tabia ya wachache wanaojilimbikizia mali na hakuogopa kufanya lolote kwa masilahi ya taifa.

Kwa mujibu wa Ngawaiya, Mrema akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alifanikisha kukamatwa kwa dhahabu uwanja wa ndege iliyokuwa inatoroshewa nje ya nchi, licha ya vitisho alivyopokea.

Ngawaiya ambaye alitoa ghorofa lake Magomeni Mapipa na kulifanya kuwa Ofisi za TLP baada ya kuhama kutoka Shauri Moyo na alipoulizwa alisema ukaribu wake na Mrema ndiyo uliosukuma kufanya hivyo.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema Mrema ana mchango mkubwa katika siasa za upinzani kwa sababu alizianza harakati hizo mara tu mfumo wa siasa za vyama vingi ulipoanzishwa.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, alisema mwanasiasa huyo, aliwahi kupata mafunzo ya ukada wa chama hicho Bulgeria na hakusita kueleza lolote lililopaswa kuelezwa pia alibuni mbinu za kudhibiti uhalifu ikiwemo kuanzisha vituo vya Polisi Kata.

Katibu Mkuu wa TLP, Richard Lymo alisema kifo cha kiongozi huyo ni pengo kwa TLP.

Spika mstaafu, Pius Msekwa alisema mwanasiasa huyo atakumbukwa kwa imani yake katika siasa za maendeleo.

Muasisi wa NCCR-Mageuzi, Prince Bagenda alisema Mrema alikuwa na shauku ya kuwa mwanasiasa na alileta mageuzi katika siasa za Tanzania.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa wa Chadema, John Mrema alisema mwanasiasa alikuwa na nguvu kiasi cha kuwaamrisha majambazi wasalimishe silaha zao na walitii amri hiyo.

Alisema hakuwa na hofu ya kujitoa serikalini na CCM kisha kuhamia upinzani ilhali alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Taarifa hii imeandaliwa na Aurea Simtowe, Juma Issihaka.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad