BOSI wa benchi la ufundi la Simba, Zoran Manojlovic ‘Maki’, ameweka wazi kuwa matakwa ya kimfumo ambao anautumia ndiyo sababu kubwa ya kutoonekana kwa straika na nahodha wa kikosi hicho, John Bocco.
Katika michezo miwili ya kwanza ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Geita Gold na Kagera Sugar ambayo Simba imefanikiwa kuibuka na ushindi, Bocco hakuwa sehemu hata ya wachezaji wa akiba na kuzua maswali huku taarifa za ndani zikieleza kuwa ni miongoni mwa wachezaji ambao hawako kwenye mipango ya kocha Maki.
Nahodha wa Simba, John Bocco.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kocha Mkuu wa Simba, Maki alisema: “Kuhusu Bocco hakuwa sehemu ya michezo yetu miwili ya kwanza dhidi ya Kagera Sugar na hii ni kutokana na mahitaji ya kimfumo ambayo tunaitumia.
“Kwenye michezo hiyo miwili iliyopita kwa nyakati tofauti tulitumia mastraika wawili, kuwa na Bocco kunamaanisha tungelazimika kutumia mastraika watatu na ni vigumu kufunga mabao ukiwa na mastraika watatu kwenye kikosi.
“Tunamtumia Moses Phiri kama nusu straika, huku Dejan Georgijevic na Habib Kyombo kwa kubadilishana na mmeona tumepata mabao matano katika michezo miwili jambo ambalo ni vigumu kulifanya ukiwa na mastraika watatu wanaocheza kwa wakati mmoja.”
Stori na Joel Thomas