TAKUKURU yaweka hadharani mbinu rushwa ya ngono vyuoni




TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga, imeweka hadharani mbinu ambazo wamekuwa wakizitumia wahadhiri vyuoni kuomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi.

Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga Donasian Kessy akizungumza na vyombo vya habari.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy, amebainisha hayo leo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa taasisi hiyo kipindi cha kuanzia robo ya nne ya mwaka wa fedha (2021/ 2022) kuanzia Aprili hadi Juni.

Amesema kwa kipindi hicho wametoa elimu maeneo mbalimbali ya mapambano dhidi ya Rushwa, ikiwamo kupinga rushwa ya ngono vyuoni mkoani humo na kubaini mbinu ambazo wamekuwa wakizitumia wahadhiri kuomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi.

“Takukuru mkoani Shinyanga tulitoa elimu ya rushwa ya ngono vyuoni kupitia kampeni ya  “Vunja ukimya kataa rushwa ya ngono”  katika vyuo vitatu ambavyo ni Veta, Ushirika, Chuo cha Maendeleo ya wananchi Buhangija na kutoa elimu kwa vijana 541,”amesema Kessy.

“Mbinu ambazo tulizibaini wanazotumia wahadhiri kwa ajili ya kuomba rushwa ya ngono kwa wanafunzi ni kuwafelisha mitihani yao kwa makusudi hasa kwa mlengwa ambaye anamtaka kimapenzi na kumtishia akifeli tena atafukuzwa chuo, na hatimaye kufanya naye mapenzi,”ameongeza.


Aidha, amesema kutokana na elimu ambayo wameitoa kwa wanafunzi vyuoni, wanatarajia kupata taarifa nyingi juu ya rushwa hiyo ya ngono, ili wawakamate wahusika na kuwachukulia hatua na kukomesha kabisa vitendo vya rushwa ya ngono vyuoni.

Katika hatua nyingine, amesema walifanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika miradi ya maendeleo 17 ya fedha za UVIKO-19 yenye thamani ya Sh.bilioni 13.7 na kubaini miradi Minne ina dosari haiendani na thamani halisi ya fedha na kuagiza ifanyiwe marekebisho.

Amesema pia walifanya uchambuzi wa mifumo kuhusiana na changamoto za ujenzi wa vyumba vya Madarasa kupitia fedha za UVIKO-19, na uendeshaji na usimamizi wa jumuiya za watumiaji maji ngazi za jamii katika Halmashauri ya Msalala, Ushetu na Kahama, na kubaini kuwepo na mianya ya Rushwa.


Amesema kwa kipindi hicho walipokea taarifa za malalamiko 29 zilizohusu Rushwa 23, Serikali za Mitaa Nane, Ujenzi Sita, Polisi Tatu, Maji Mbili, Elimu Mbili, Biashara Mmoja, Afya Mmoja, na taarifa 18 uchunguzi wake unaendelea, Tano uchunguzi umekamilika, kesi Saba zinaendelea Mahakamani.

Nao baadhi ya wanafunzi ambao wanasoma Chuo cha St. Joseph Tawi la Shinyanga, wamekiri ni kweli baadhi ya wahadhiri wamekuwa wakiwaomba Rushwa ya ngono na hata kuwafelisha masomo yao ili wakubali kufanya nao mapenzi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad