Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania, Nevile Meena amesema kosa la kitaalamu na madai yasigeuzwe kuwa ya jinai bali bodi za kitalaamu ndizo zilishughulikie na kutoa adhabu.
Meena ametoa kauli hiyo, wakati akizungumzia juu ya mchakato wa marekebisho ya sheria za huduma za habari unaotarajia kufanywa na Serikali baada ya kupokea maoni kutoka kwa wadau wa sekta ya habari siku chache zilizopita jijini Dar es Salaam.
“Mimi hata sijui kwa nini Serikali ilipokuwa ikitunga sheria hizi mwaka 2016 iliamua kuweka kosa la kitalamu linalofanywa na wanahabari ni jinai, sisi tunaona hii si sawa na tumeshapeleka mapendekezo yetu tukitaka kosa la kitalaamu lishughulikiwe kitaalamu” amesema
Meena amesema kama zilivyo taalamu nyingine zina bodi na vyombo vinavyowaongoza ambapo pia hushughulika na makosa yanayofanywa na wanataalamu husika tofauti na makosa ya wanahabari yaliyogeuzwa ni jinai.
Meena amesema madai ya kashfa kwa mwanahabari yanageuzwa na kuwa kosa la jinai yanatoa taswira mbaya ndani na nje ya nchi lakini pia yanaua tasnia ya habari.
“Sinaona nchi yoyote madai ya kashfa yameguzwa ni jinadi zaidi ya hapa kwetu, lakini naamini Sheria ya huduma za Habari ya Mwaka 2016 itakafinyiwa marekebisho makubwa kama tulivyopendekeza” amesema
Meena pia amesema miongoni mwa mambo waliyoyapendekeza ni kufikishwa mahakamani kwa wadaiwa wote ambao licha ya kukumbushwa kulipa madeni wanayodaiwa na vyombo vya habari kwa miezi sita hajalipa.
Amesema naamini vyombo vya habari vikiwa na uwezo mzuri wa kujiendesha na kuwalipa vizuri watumishi wake lawama za kukosekana kwa weledi na uzalendo zitapungua.
“Suala la mapendekezo yote ya wadau wa habari kupita, hilo ni suala lingine. Cha msingi ni kwamba, miongoni mwa ahadi za Rais (Samia), ikiwemo wizara kukutana na wadau wa habari na kupitia vifungu, imetekelezwa.
Mwandishi wa habari wa kujitegemea, Said Muslimu amesema anaamini muswada wa mabadiliko ya sheria ya huduma za vyombo vya habari utapelekwa bungeni katika vikao vya Bunge vijavyo.
“Serikali hii imekuwa tofauti na iliyopita, haya mapendekezo ya wadau yanaonekana yana Baraka za viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ambaye kila wakati amekuwa akitutia moyo na kutaka tusahau yaliyopita” amesema
Mwandishi wa Mwananchi, Baraka Loshilaa, amesema anaamini sheria zitakazofanyiwa marekebisho hazitampa waziri mamlaka ya kufuta leseni au kufungia chombo cha habari
“Chombo cha habari kinapofungiwa kwa kosa la mtu mmoja au wawili wanaoumia ni wengi hivyo ni vema mabadiliko yafanyike ili adhabu iwaguse wachache waliohusika na kosa na wengine waendelee na uzalishaji” amesema.