KAMANDA wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilbrod Mutafungwa, amemwagiza Ofisa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kitengo cha utoaji wa leseni kwa kushirikana na polisi kutoa leseni za udereva kwa madereva wenye sifa na vyeti vinavyotambulika kisheria.
KAMANDA wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilbrod Mutafungwa.
Alisema, watakapowabaini madereva wana leseni na wamezipata kwa njia ya panya, Idara ya Ukaguzi wa Jeshi la Polisi na Ofisa ya utoaji wa leseni TRA, watawajibishwa kisheria.
Kamanda Mutafungwa alisema wamebaini madereva wengi wanaosababisha ajali nyingi wana leseni walizozipata kwa njia za udanganyifu.
Alibainisha hayo jana wakati wa Tamasha la Elimu ya Usalama Barabarani kwa watumiaji wa barabara lililofanyika kitaifa wilayani Kahama, mkoani Shinyanga katika viwanja vya kituo kidogo cha mabasi CDT kwa kushikisha viongozi mbalimbali wakiwamo wa madhehebu ya dini.
Alisema, madereva wengi wanaoendesha vyombo vya moto wana leseni bila kuwa na vyeti vinavyoonesha amesomea udereva kwenye chuo kinachotambulika na zinatolewa kwa njia za panya ilhali wahusika wanafahamu kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sheria za usalama barabarani.
“Mahakama zetu ziendelee kutoa adhabu kubwa kwa madereva wanaofikishwa mahakamani kwa makosa ya uvunjaji wa sheria za usalama barabarani, faini zinazotolewa kwao wanaziona za kawaida hivyo lazima wafungwe ili iwe fundisho kwao,” alionya Mutafungwa.
Pia, alimtaka Mkuu wa Usalama Barabarani mkoani Shinyanga, SSP Debora Lucas, kwa kushirikiana na askari wake, kufanya ukaguzi wa mabasi yote yanayobeba wanafunzi katika shule binafsi na yatakayobainika kuwa mabovu kuyatoa namba za usajili mpaka yatakaporekebishwa.
Alisema, ajali nyingi za mabasi ya wanafunzi zinatokea kwa uzembe wa madereva, ubovu wa mifumo ya breki, mataili vipara na yatayokuwa safi baada ya ukaguzi wamiliki wapate vyeti vitavyoonyesha magari yao yamekaguliwa na yako salama kubeba wanafunzi na kuagiza lifanyike kabla ya shule kufunguliwa.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani wilayani hapo, Idsam Mapande alisema, mawakala wa mabasi ni chanzo cha ajali barabarani kwa kucheza michezo ya kubahatisha baina yao na madereva wa mabasi yanayofanya safari za mikoani kwa Sh. 500,000.