Wasanii Tundaman pamoja na Stan Bakora wakiomba radhi mbele ya waandishi wa habari
KUFUATIA shutma nyingi na malalamiko dhidi yake kwa kile alichokifanya wakati akitumbuiza kwenye kilele cha tamasha la Simba Day, leo Agosti 11 2022 msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya Tundaman akiambatana na msanii mwenzie Stan Bakora wamejitokeza hadharani ili kuelezea na kutoa utetezi wake kwa shutma zinazomkabili.
Tundaman ametanabaisha kuwa walichokifanya kwenye kilele cha sherehe za Simba Day hakikulenga kwa namna yoyote ile kudhihaki madhehebu ya dini ya kikristo na lengo lao halikuwa kusababisha mfadhaiko kwa waumini wa dini hiyo.
Tundaman aliendelea kwa kusema kuwa lengo lilikuwa ni kuonesha ubunifu katika kazi yake ya sanaa na walilenga zaidi kwenye kuburudisha huku wakiwafanyia utani watani wa klabu hiyo ya Simba ambao ni klabu ya Yanga.
Wasanii hao wamesema kuwa hawakuwa na nia yoyote ya kudhihaki dini au imani ya watu
Msanii Stan Bakora alidakia na kusema kwa utani: “Nadhani pia wosia ndio uliowakera sana watu wa Yanga maana wengi waliomaindi ni mashabiki wa Yanga, Ingawa ni kweli tumegusa maswala ya kiimani”.
Tundaman Alimalizia kuomba radhi kwa kusema:
“Kwa unyenyekevu mkubwa na kwa maslahi mapana ya maendeleo ya Sanaa ya nchi kwa ujumla ningependa kuomba radhi kwa viongozi wote wa madhehebu ya kikristo, waumini wa dini ya kikristo, Baraza la Michezo, Baraza la Sanaa, wadau pamoja na jamii yote kwa ujumla kutokana na maudhui niliyotumia kwenye tamasha la Simba day endapo itakuwa nimewakwaza kwa namna moja au nyingine, kwani lengo langu lilikuwa ni kuonesha ubunifu wangu wa kisanaa na si kudhihaki Imani au dini ya mtu yeyote.”
Imeandikwa: Abdallah Ally kwa msaada wa mitandao