Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamadi Masauni ameagiza kufanywa uchunguzi wa kina ili kubaini mauaji ya kinyama dhidi ya watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni wachimbaji wa madini ambao miili yao ilikutwa kwenye viroba na kutupwa kwenye kijiji cha Lusane kata ya Tunguli Mkoani Tanga
Watu hao wamekutwa wakiwa na majeraha mbalimbali yanayosadikiwa yalitokana na kupigwa na nondo huku shingo zao zikiwa zimevunjwa
Waziri Masauni ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara wilayani humo katika hospitali ya Teule mahali ambapo miili ya watu hao imehifadhiwa, ziara aliyoifanya akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba amesema tukio hilo limeuchafua Mkoa wa Tanga huku akisema vyombo vya dola vitashirikiana kuwabaini wahusika wa tukio hilo.
Viongozi mbalimbali walioshiriki kwenye ziara hiyo akiwemo Mbunge wa jimbo hilo Omari Kigua, Mkuu wa Wilaya hiyo Abel Busalama, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tanga, Safia Jongo wamelaani tukio hilo.
Miili hiyo bado haijafahamika licha ya picha zao kuoneshwa kwenye machimbo mbalimbali ya madini katika wilaya ya Kilindi, kwa lengo la kubaini ndugu na jamaa wa karibu wa watu hao