Uhuru Ajipata Njia Panda Harakati za Kumzika Naibu Wake Ruto



Uhuru ajipata njia panda
RAIS Uhuru Kenyatta yumo kwenye njia panda katika juhudi za kumzima naibu wake William Ruto kumrithi.

Hii ni baada ya juhudi za kabla ya uchaguzi, uchaguzi na kutangazwa kwa matokeo kushindwa kuzuia Dkt Ruto kutangazwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Matumaini ya Rais Kenyatta sasa yamo kwa Mahakama ya Upeo akitarajia itafuta ushindi huo.

Hii ni baada ya mwaniaji urais wa Azimio, Raila Odinga kwenda kortini kupinga ushindi wa Dkt Ruto kwa misingi kuwa Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati “alihujumu” uchaguzi wa urais.


Rais Kenyatta amekuwa kimya tangu IEBC kumtangaza Dkt Ruto kama Rais Mteule wiki mbili zilizopita. Hii ni licha ya baadhi ya marais wa mataifa tofauti barani Afrika na duniani kumtumia Dkt Ruto jumbe za heri njema.

Wadadisi wa siasa wanasema kimya cha Rais Kenyatta kimechangiwa na kutotimia kwa mpango wake wa kisiasa, ikizingatiwa alikuwa akimuunga Bw Odinga kuwa mrithi wake.

“Rais Kenyatta anaonekana bado kushangazwa na jinsi mrengo wa Ruto ulivyoibuka mshindi, ikizingatiwa alikuwa katika mstari wa mbele kumfanyia kampeni Bw Odinga. Vile vile, amekuwa akisisitiza Ruto hakufaa kuchaguliwa,” asema Bw Dismus Mokua, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.


Kabla ya uchaguzi kufanyika, Rais Kenyatta alikuwa katika mstari wa mbele katika mikakati iliyolenga kutibua juhudi za Dkt Ruto, kuu ikiwa ni kubuniwa kwa muungano wa Azimio. Baada ya muungano huo kubuniwa, Rais Kenyatta alichukua wadhifa wa mwenyekiti wa Azimio na kuongoza maafisa wa serikali kumpigia debe Bw Odinga.

Katika kampeni kali alizoongoza Rais Kenyatta dhidi ya naibu wake, maafisa kadhaa wa ngazi za juu serikalini walijiunga naye kumpiga vita Dkt Ruto. Baadhi yao ni mawaziri Joe Mucheru (ICT), Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani) na Keriako Tobiko (Mazingira) pamoja na Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Karanja Kibicho.

Rais Kenyatta alianza juhudi za kumzima naibu wake mnamo 2018 alipoingia handisheki kati yake na Bw Odinga pamoja na Mpango wa Marekebisho ya Katiba (BBI).

MPANGO WA BBI

Dkt Ruto aliongoza kampeni kali kupinga mpango huo, akishikilia kwamba ulikuwa njama ya siri ya Rais Kenyatta na washirika wake kuongeza nyadhifa kuu serikalini.


“Ni wazi kuwa Rais Kenyatta aliweka kila juhudi kuhakikisha BBI imepita ili kufanikisha mikakati yake ya kisiasa. Kufutiliwa mbali kwake na mahakama kulikuwa pigo kubwa ambalo liliongeza uadui baina yake na Ruto,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Juhudi zaidi za kuzuia Dkt Ruto kuongoza Kenya zilishuhudiwa katika ukumbi wa Bomas kabla yake kutangazwa Rais Mteule.

Kulingana na nakala ya kiapo ya Bw Chebukati kwenye kesi ya kupinga ushindi wa Dkt Ruto katika Mahakama ya Upeo, maafisa wa ngazi za juu serikalini walijaribu kushinikiza IEBC kutomtangaza Dkt Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Bw Chebukati anadai kwenye nakala hiyo ya kiapo kuwa mwendo wa saa nne za asubuhi siku ya kutangazwa kwa matokeo ya urais mnamo Agosti 15, ujumbe wa serikali ulienda Bomas ukidai kuwa machafuko yangezuka nchini iwapo Dkt Ruto angetangazwa mshindi.


Ujumbe huo, kulingana na Bw Chebukati uliongozwa na Waziri Msaidizi katika Ofisi ya Rais Kennedy Kihara, Wakili Mkuu wa Serikali Kennedy Ogeto, Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai na Naibu Mkuu wa Majeshi Francis Ogolla.

Bw Chebukati anadai Bw Kihara alimwambia walitumwa na Kamati ya Usalama wa Kitaifa (NSAC) kumwambia kuwa akitamtangaza Dkt Ruto kuwa mshindi kungezuka machafuko nchini, na kuwa tayari fujo zilikuwa zimelipuka katika mitaa ya mabanda ya Kibra na Mathare.

Mwenyekiti huyo wa IEBC anaeleza kuwa Bw Kihara alimtisha kuwa makamishna wangebeba mzigo wa ghasia ambazo zingezuka kwa kumtangaza Dkt Ruto kuwa Rais Mteule.

Anasema ujumbe huo pia ulimwambia ikiwa ingekuwa vigumu kumtangaza Bw Odinga kuwa mshindi wa urais, basi ni lazima wangetangaza matokeo ambayo yangehakikisha kuna duru ya pili ya uchaguzi wa urais.

Bw Chebukati anasema aliambia ujumbe huo kuwa hangetekeleza matakwa yao kwani alikuwa na jukumu la kuzingatia Katiba.


Wadadisi wa siasa wanasema Wakenya na hata washirika wa Kenya kimataifa wanatarajia kuona hatua ambayo Rais Kenyatta atachukua baada ya uamuzi wa Mahakama ya Upeo wiki ijayo, moja ikiwa ni iwapo atakuwa radhi kukabidhi madaraka kwa Dkt Ruto iwapo majaji watashikilia tangazo la IEBC.

Ndoa kati ya Kenya Kwanza na vyama vya Azimio ni haramu...


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad