Ukaguzi Magari ya Shule Waja




Dar es Salaam. Siku chache baada ya gari la Shule ya Msingi King David mkoani Mtwara kupata ajali na kuua watu 13, wakiwemo wanafunzi 11, Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani limejipanga kuanza kutoa elimu kwa madereva na ukaguzi wa mabasi yote ya shule.

Ajali hiyo ilitokea asubuhi ya Julai 26 mwaka huu, katika eneo la Mjimwema, Kata ya Mikindani, Mtwara Mjini wakati wanafunzi hao wakipelekwa shule.

Gari lililokuwa limewabeba wanafunzi zaidi ya 25 ni aina ya hiace, hali iliyosababisha mijadala, ikiwemo ukubwa na gari na idadi ya wanafunzi na iwapo halikuwa na tatizo.

Hoja nyingine iliyoibuliwa na wadau ni baadhi ya magari ya wanafunzi kuwa mabovu.


Jana, Kamanda wa Usalama Barabarani nchini, Wilbrod Mutafungwa akizungumza na gazeti hili kuhusu hoja hizo, alisema kutokana na changamoto hiyo wameona kuanzishwe ukaguzi nchi nzima.

“Tutatumia fursa hii ya shule nyingi kufungwa kukagua magari yote na kuyarudia tena na tutafanya hivi kwa mwezi mmoja,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Alisema wanatarajia kuanza shughuli ya ukaguzi huo kuanzia kesho kwa kila mkoa.

“Utakuwa ni ukaguzi wa magari na kutoa elimu kwa wasimamizi na madereva na mkoa wa Dar es Salaam, shughuli hiyo itafanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia saa mbili asubuhi na tunaomba wote wajitokeze,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Hassan Mchanjama alisema jeshi hilo lilikuwa limejisahau na walikuwa hawafuatilii mabasi yanayobeba wanafunzi, lakini baada ya ajali kutokea wameanza kushtuka.

“Naamini hii itakuwa shughuli endelevu na siyo zimamoto,” alisema Mchanjama
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad