Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amemwamuru Padri Christopher Fosudo, ambaye ni raia wa Nigeria, kuondoka mara moja jimboni mwake na kurejea nchini kwao.
Padri Fosudo (pichani) alikuwa paroko msaidizi, Parokia ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda, Magomeni Dar es Salaam, huku taarifa za kufukuzwa kwake zikiibua maswali mbalimbali.
Viongozi mbalimbali wa kanisa hilo walikuwa wagumu kuzungumzia suala hilo la kiongozi huyo wa kiroho kutakiwa kuondoka nchini, huku baadhi ya waumini wa parokia hiyo wakionyesha kushtushwa na taarifa kwamba alikuwa paroko wao msaidizi.
Barua iliyotumwa kwa mapadri wote jimboni humo kuhusu kufukuzwa kwa Padri Fosudo, ilianza kusambaa juzi jioni mitandaoni ikiwa na saini ya Katibu wa Askofu, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Vicent Mpwaji.
Sehemu ya barua hiyo inasomeka, “Askofu Mkuu wa Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi OFMCap anatoa taarifa kwamba Padri Christopher Fosudo kutoka Nigeria ambaye alikuwa anahudumu hapa jimboni kama Paroko Msaidizi wa Parokia ya Magomeni, hatakiwi tena kuwepo hapa jimboni Dar es Salaam.
“Hivyo, Askofu Mkuu amemuagiza Padri Fosudo arudi nchini kwake Nigeria,” inasomeka barua hiyo ya Agosti 17 mwaka huu.
Gazeti hili lilimtafuta Padri Mpwaji kwa simu kutaka kujua usahihi wa barua hiyo, lakini alisema: “Sina ‘comments’ (maoni) kwa suala hili.”
Alipoulizwa kama barua hiyo ni ya kwake au la, Padri Mpwaji alisema: “Naomba hili libaki kama lilivyo.”
Padri Mpwaji alimhoji mwandishi: “Barua hiyo imeelekezwa kwa nani?” ambapo alijibiwa kuwa ni kwa mapadri wote. Hapo ndipo aliposisitiza akisema: “Basi itabaki kuwa hivyo”.
Majibu hayo yalilifanya gazeti hili kumtafuta kwa simu Askofu Mkuu Ruwai’chi, ambaye alisema asingeweza kuweka wazi sababu, huku akimuuuliza mwandishi barua hiyo imeelekezwa kwa nani, akajibiwa kwa mapadri kisha akasema: “Mimi nimepeleka ujumbe kwao.”
Alipoulizwa kama utaratibu wa kumwondoa jimboni kwake umekwisha kufanyika, kiongozi huyo wa kiroho alisema: “Hilo mtafuteni mwenyewe.”
Hata hivyo, jitihada za kumpata Padri Fosudo kuzungumzia suala hilo la kufukuzwa jimboni hazikuzaa matunda, kwani juhudi za kumpata hata kupitia simu ya mkononi hazukuzaa matunda.
Mwananchi lilimtafuta Paroko wa Parokia ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda, Magomeni, Padri Christian Likoko, ambaye naye alisema asingeliweza kuzungumza lolote kuhusu suala hilo, bali aulizwe aliyeandika barua hiyo.
Awali, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima alisema suala hilo ni la kijimbo, hivyo watafutwe wahusika wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Padri mmoja aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutokutajwa jina alisema, Padri Fosudo amewahi pia kufundisha katika Chuo Kikuu cha Jordan kilichopo mkoani Morogoro.
“Hata kabla ya kuja Jimbo Kuu la Dar es Salaam, aliwahi kuhudumu kwa muda katika Jimbo Kuu la Dodoma katika Kanisa Kuu la Mt Paulo wa Msalaba na haikufahamika mara moja alikwenda wapi baada ya hapo,” alisema padri huyo na kuongeza:
“Alipotoka Jordan alikwenda kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ingawa sikujua alikwenda kusoma kozi gani. Amepata pia kuhudumu kwa muda pale Parokia ya Manzese (Dar es Salaam).”
Kutokana na taarifa za kutakiwa kuondoka, gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Uhamiaji, Paul Mselle kujua kama Padri Fusudo amekwisha kuondoka nchini, alisema wameanza kufuatilia suala hilo.
“Taarifa hiyo tumeiona tu mitandaoni, hatujapata taarifa kamili lakini Magomeni iko Kinondoni, ofisi hiyo hiyo ya Kinondoni imeanza kufuatilia,” alisema Mselle.
Mmoja wa waumini wa Parokia hiyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake alisema, ameona taarifa hiyo, “Lakini nashangaa kusikia alikuwa paroko msaidizi. Sisi tulikuwa tukimwona akija na kuondoka.
“Hili la yeye kuwa paroko msaidizi kwa kweli limenishtua. Lakini sababu hasa iliyofanya akafukuzwa bado inabaki gizani na ingependeza tukawekwa wazi, kwani alikuwa padri wetu,” alisema.
Hali ilivyokuwa kanisani
Jana, gazeti hili lilikwenda Parokia ya Magomeni kuona kinachoendelea na kuwakuta waumini wa kanisa hilo wakiwa kwenye vikundi vikundi, huku mmoja wa hao akisikika akisema ameshikwa na butwaa kuona barua hiyo ikisambaa mitandaoni.
Wakati muumini huyo akishtuka, mwingine aliyekuwa kando alimweleza aliyoyaona kwenye mitandao ni ya kweli, “na unajua anapaswa kuondoka.”
Baada ya kuzungumza hivyo ndipo mmoja katika kundi hilo ambaye ni mwanamume alisema sasa waliokuwa hawana furaha leo hii watakuwa na furaha kwa sababu Padri Foduso ameondolewa.
Muumini mwingine ambaye alikuwa mwanamke yeye alikumbushia tukio la mwezi uliopita kwamba wakati akiendesha misa, ilipofika katikati ya misa, Paroko alikatishwa na kuamriwa atoke nje.
“Huyu father (padri) hapendi kujichanganya na wenzake, ndivyo ninavyomjua yaani ana katabia fulani hivi, yaani kwa mtu wa kawaida huwezi... Nilikuwa simuelewi hata kidogo,” alisema muumini akimwelezea padri huyo.