Uteuzi wa Majaji Wazua Gumzo




Dar es Salaam. Licha ya wanasheria kupongeza uteuzi wa majaji 22 wa Mahakama Kuu uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, wamependekeza mageuzi yatakayoufanya mchakato wa kuwapata watoaji hao wa haki kuwa wa wazi kuliko ilivyo sasa.

Ukiondoa mteule mmoja ambaye awali alikuwa mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu usiku wa kuamkia jana, ilionyesha mawakili wa Serikali, mahakimu waandamizi, mawakili wa kujitegemea na wahadhiri wa vyuo vikuu, wakiwa miongoni mwa walioteuliwa kushika wadhifa huo muhimu katika utoaji wa haki.

Uteuzi huu umevunja rekodi kwa kuwa wenye idadi kubwa ya majaji wa Mahakama Kuu waliowahi kuteuliwa kwa mara moja.

Mei mwaka jana, Rais Samia aliteua majaji saba wa Mahakama ya Rufani na wengine 21 wa Mahakama Kuu.


Rekodi ya mwisho ya uteuzi wa majaji wengi kabla ya Rais Samia ilifanywa Agosti 2014 na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete baada ya kuteua majaji 20 wa Mahakama Kuu kwa mpigo.

Rais Samia ameweka pia historia kwa kuchagua majaji wengi wanawake kwa wakati mmoja kuliko ilivyokuwa kwa watangulizi wake. Majaji 10 kati ya 22 walioteuliwa ni wanawake na uapisho wao utafanyika siku yoyote.

Uteuzi huo pia unafanya idadi ya majaji wa Mahakama Kuu kufikia 111 kutoka 89 waliokuwepo awali.


Hisia tofauti

Uteuzi wa jana umevuta hisia za wanasheria, wanaharakati na wanasiasa, ambao licha ya kuelezea ni hatua muhimu katika kuharakisha utoaji haki, wametaka utaratibu wa kuwapata majaji uboreshwe na kuwa wa wazi zaidi.

“Hatua hii ni nzuri, itapunguza mrundikano wa kesi Mahakama Kuu, lakini tungependa kuona mchakato huu wa kuwapata majaji unakuwa mzuri zaidi. Watu wasailiwe kama Kenya. Wanaotaka nafasi hiyo waombe na rekodi zao zinawekwa hadharani,” alisema wakili wa kujitegemea, Dk Rugemeleza Nshalla.

Nshalla ambaye aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ameonyesha pia kutoridhika na idadi ndogo ya mawakili wa kujitegemea walioteuliwa kuwa majaji.

“This time (zamu hii) mawakili wa kujitegemea ni wawili tu, tulitegemea wawe zaidi, lakini mwishowe na kwa sheria tuliyonayo, Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteua,” alisema.


Wakili mwingine mwandamizi, Francis Stolla alisema majaji walioteuliwa wana sifa za ujaji zilizoainishwa kwenye Katiba, na kwamba wingi wao utasaidia kupunguza mrundikano wa kesi.

Kwa mujibu wa Ibara ya 109 (7) mtu anaweza kuteuliwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu endapo ana sifa za kuwa wakili kama zilivyotajwa katika Sheria za Mawakili ambazo lazima mtu awe na mojawapo ya sifa hizo ili aweze kukubaliwa kuwa wakili Tanzania Bara.

Sifa hizo ni pamoja na kuwa na shahada ya kwanza ya sheria inayotambuliwa na mamlaka ya ithibati. Pia awe ni mtu aliyefaulu mtihani wa Baraza la Elimu ya Sheria (CLE).

Sifa nyingine ya kuweza kuchaguliwa kuwa jaji ni kuwa hakimu ambaye amekuwa na sifa za kuwa wakili Tanzania kwa muda usiopungua miaka 10 au awe na sifa za kuwa wakili.


Mjadala wajumbe tume za uchaguzi

Katika uteuzi huo wamo waliokuwa watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ambao uteuzi wao umeibua mjadala.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliandika kwenye akaunti yake ya twitter kuwa kuwapa ‘tuzo ya ujaji’ anaowahusisha na kile anachoamini kuvuruguka kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, si sawa.

Hata hivyo, wakili Stolla anaona kuwa uteuzi wa wajumbe hao wa NEC na ZEC, hauwezi kuathiri utoaji haki, endapo wateule hao watatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

“Unajua kwenye Katiba kuna doctrine (dhana) inaitwa independence of the judiciary (uhuru wa mahakama). Hii ni moja ya fundamental principal (kanuni ya msingi) ya rule of law (utawala wa sheria). Ili mahakama iwe huru majaji lazima wapewe majukumu ya mahakama, hatakiwi kupewa majukumu ya kiserikali.

“Mishahara yao pia inatoka kwenye fuko kuu la hazina ili kuondoa shaka wanaweza kuingiliwa na wenye fedha na pia majaji wamepewa security of tenure, sasa hivyo vyote ni independence of the judiciary. If a judge is that much independent (jaji akiwa huru kwa kiwango hicho), hatarajiwi kufanya kazi kwa upendeleo,’’ alisema na kuongeza:


“Kama jaji ana weaknesses (kasoro) zake basi hizo ni personal weaknesses of that particular judge (kasoro zake kama jaji) na si institutional (kasoro za kitaasisi) weakness. Jaji akiamua kumwogopa aliyemtuma au kuamua kesi kwa kumwogopa aliyemtuma, huo ni udhaifu wake,” alisema Stolla.

Pia alisema: “Kwangu mimi mtu kama alikuwa NEC au ZEC ni mfanyakazi tu wa dola kama vile ambavyo alikuwa kwenye ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au wizarani. Ikitokea akaamua kesi kwa sababu anaona uteuzi ni fadhila, basi huo ni udhaifu wake, hata mtu ambaye hakuwa huko anaweza kufanya hivyo,” aliongeza.

Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe alisema uteuzi wa majaji 22 ni jambo sahihi lililokuwa kwa muda sahihi, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza mrundikano wa kesi.

“Kitu kingine cha pekee katika uteuzi huu ni idadi ya kina mama, tunaona uwiano wa kijinsia umezingatiwa,” alisema Massawe.

Aliongeza kusema kuwa ongezeko hilo la watendaji wa mahakama, linakwenda sambamba na maboresho makubwa ya miundombinu yanayofanywa na mahakama.

“Unapoboresha majengo na miundombinu mingine ya mahakama, lazima pia uongeze na rasilimali watu,” alisema.

Hata hivyo, naye hakubaliani na madai kuwa kuteuliwa kwa wajumbe wa NEC na ZEC ni zawadi ya kisiasa, hivyo kunaweza kuathiri utoaji haki.

“Haikataliwi mtu kuwa na hisia, lakini walipopelekwa ni taasisi huru. Sidhani kama uteuzi wao utaathiri kitu japokuwa watu hawazuiwi kuwaza. Kinachozingatiwa awe na sifa na uhuru wa kutosha.

“Katiba imetaja sifa za mtu kuwa jaji wa Mahakama Kuu. Jaji akionesha tatizo la kimaadili basi litachukuliwa kuwa ni individual (binafsi) na si la taasisi.”

Kama ilivyokuwa kwa Nshalla, Massawe alipendekeza mfumo wa kuwapata na kuwateua majaji uboreshwe ili uwe wa wazi.

“Kwenye hii dunia ya uwazi ni vema tungeboresha na wanaoomba nafasi hiyo wafanyiwe usaili na wateuliwe kwa vigezo na sifa kuondoa watu kukosa imani na mfumo wa uteuzi,” alisema.

Aidha, uteuzi huo umeshuhudia Gabriel Pascal Malata aliyekuwa Wakili Mkuu wa Serikali akiwa miongoni mwa wateuliwa.

Malata amehudumu nafasi hiyo kuanzia Julai 10, 2020 alipoteuliwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli. Malata alikuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.

Taarifa hiyo imesema kuwa tarehe ya kuapishwa majaji hao wateule itatangazwa baadaye.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad