Dar es Salaam. Mikiki mikiki ya ligi mbalimbali duniani iliendelea wikiendi iliyopita na kuleta msisimko kwa mashabiki wa soka.
Ligi Kuu ya England, kuanza kwa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), Ligi kuu ya Ujeruman (Bundesliga) na mechi ya Ngao ya Jamii ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambapo’ moto’ uliwaka kati ya Yanga na Simba.
Matukio ya kutatanisha yalitokea katika michezo mbalimbali na kusabisha wachezaji, makocha, viongozi wa timu na mashabiki kulalamikia.
Ukiachana na vurugu za makocha Thomas Tuchel wa Chelsea na Antonio Conte wa Tottenham, pia kuna tukio linalomuhisisha mshambuliaji Kai Havertz wa Chelsea dhidi ya Rodrigo Bentancur .
Na pia rafu ya mchezaji wa Simba Henock Inonga Baka kwa kiungo wa Yanga, Salum ‘Sureboy’ Abubakar.
Matukio yote haya yanahitaji kufanyiwa ufafanuzi wa kina kwa mujibu wa sheria Fifa.
Tuchel vs Conte
Ni mara chache makocha kuonyeshwa kadi nyekundu kwa ‘utovu’ wa nidhamu katika soka. Ni tukio la kushangaza ambalo limekuwa gumzo kwa mashabiki wa soka duniani na wengine kuhoji kuna’ vita’ gani dhidi yao.
Inawezakana kuna mahali mmojawao alifanya jambo la kumkwaza mwenzake, lakini katika mpira wa miguu, moja ya nguzo kubwa ambayo mashabiki wa soka na viongozi wanatakiwa kuwekeza mkazo ni ‘fair play’ na nidhamu.
Katika mchezo uliowakutanisha makocha hao, Conte alimfuata Tuchel kumpa ‘fair’ baada ya mwamuzi Anthony Taylor kupuliza filimbi ya mwisho wa mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Tuchel alimshika mkono Conte na mkuvuta kwa ‘jazba’, jambo lililosababisha Conte kuhamaki na kusababisha vurugu ambayo iliwafanya wachezaji na maofisa wengine kuingilia kati na kuwaamua.
Hali hiyo ilimfanya mwamuzi Taylor kuwaadhibu makocha hao kwa kadi nyekundu. Awali makocha hao walionyeshwa kadi za njano kwa ukosefu wa nidhamu.
Kai Havertz vs Rodrigo
Totteham Hostspur walisawazisha bao kupitia Pierre-Emile Hojberg katika dakika 68 ya mchezo, bao ambalo limewaibua wachezaji wa zamani wakilalamikia maamuzi ya Taylor na waamuzi wa VAR kwani kabla ya tukio la kufunga bao, mchezaji Bentancur alidaiwa kumfanyia rafu Havertz.
Kiungo wa zamani wa timu ya Taifa ya Hispania, Francesc “Cesc” Fabregas Soler alishangazwa na maamuzi ya Taylor ambaye awali mashabiki wa timu hiyo walimpinga mara baada ya kutangazwa na FV kuwa atachezesha mechi hiyo.
Inonga vs Sure Boy
Mchezaji wa Simba Henock Inonga alimfanyia rafu mbaya kiungo mshambuliaji wa Yanga, Sureboy katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza katika mchezo wa Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa Jumamosi Agosti 13, 2022.
Baada ya rafu hiyo, Sure Boy aliamka na kumvamia Inonga ambaye baadaye alianguka chini. Mwamuzi aliwaonya kwa kadi ya njano kila mmoja.
SHERIA ikoje?
Kwa mujibu wa Fifa na bodi ya kutunga sheria za soka (IFAB) sheria namba 5.3 mwamuzi amepewa mamlaka ya kuwaadhibu maofisa wa timu na wachezaji.
Maofisa hao ni pamoja na kocha mkuu, kocha msaidizi, meneja, daktari na maofisa wengine kwa mujibu wa sheria.
Mwamuzi anaweza kuwaonya kwa kadi ya njano na nyekundu na kutumikia adhabu kwa mujibu wa sheria za soka.
Tuchel na Conte wameshindwa kujizuia na kutenda vitendo vya utovu wa nidhamu na adhabu yao watakosa mechi moja ya mashindano yanayosimamiwa na FA.
Adhabu hiyo ni tofauti na ile aliyopewa Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi ambaye mbali ya kufungiwa mechi tatu, alitozwa faini kwa mujibu wa sheria za TFF.
Nabi hakushikana mashati na kocha mwenzake zaidi ya kumlalamikia mwamuzi wa akiba!.
Mchezaji wa Tottenham Bentancur hakumfanyia rafu Havaertz kwa mujibu wa picha za marejeo za VAR. Bentancur alifanikiwa kuucheza mpira huku Havertz akimuangukia na kulifanya tukio hilo kuwa siyo rafu. Ingekuwa rafu endapo mguu wa Bentacur ungegusa wa Havertz na kumfanya mwamuzi kuwa sahihi katika maamuzi.
Wadau wa soka walimtarajia mwamuzi Elly Sasii angemuadhibu kwa kadi nyekundu Inonga kwa ‘rafu’ aliyoifanya kwa Sure Boy kwa mujibu wa sheria namba 12 ya Fifa na IFAB. Hata hivyo, kitendo cha mwamuzi kutoa kadi ya njano kwa Inonga ilikuwa kwa ajili ya ‘Spirits of the Game’ na lengo hilo lilitimia baada ya matokeo ya ushindi wa Yanga wa mabao 2-1 na kutwaa Ngao ya Jamii. Kwa upande wa Sure Boy, alipaswa kupewa kadi ya njano (kama mwamuzi alivyofanya) na hiyo imetokana na kitendo cha kumvamia Inonga. Busara’ ilitumika zaidi katika kutoa maamuzi ya tukio hilo na kufanikisha mechi hiyo kumalizika salama pamoja na hoja katika mitandao ya kijamii.