AJALI mbaya iliyohusisha magari manne imetokea leo katika eneo la Shamwengo huko Mbeya ikisababisha vifo kwa watu zaidi ya nane huku idadi ikihofiwa kuongezeka na idadi ya majeruhi ikiwa bado haijawa wazi.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya Urich Matei amesema chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni kufeli kwa breki ya lori lenye namba za usajili T387 DFJ lililobeba mchanga unaosemekana kuwa ni madini likielekea bandarini.
Baada ya kufeli breki katika eneo hilo lenye mteremko lori hilo liligonga magari kadhaa ikiwemo basi la abiria la Super rogers na kusababisha vifo na majeruhi kwa baadhi ya abiria, pia liligonga gari ndogo aina ya marcedes na kugonga Lori jengine kabla ya kupoteza uelekeo na kutoka nje ya barabara.
Kamanda ameongezea kwa kusema kuwa taarifa zaidi kwa majeruhi na vifo zitaendelea kutolewa kufuatia ajali hiyo huku akihimiza umakini wa watumiaji wa vyombo vya moto katika kuhakikisha usalama wa vyombo vyao kabla ya kuanza safari pamoja na kuweka wazi mpango wa jeshi la polisi wa ukaguzi wa malori kabla ya kuanza kushuka kwenye mteremko uliopo katika eneo hilo.