Vipimo vya UTI ni balaa "Kila Nikienda Kupimwa Nakutwa na UTI"




Dar es Salaam. “Kila nikihisi homa na kwenda hospitali kupima nakutwa na UTI. Imekuwa ikinitokea mara kwa mara, napewa dawa nakunywa lakini bado inarudi tena,” ni kauli ya Mwanahamisi Ally, mkazi wa Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Urinary Tract Infection au UTI ni ugonjwa unaosababishwa na maambukizi kwa njia ya mkojo na huwaathiri zaidi wanawake na watoto, na Mwanahamisi ni mmoja kati ya wananchi wengi wanaolalamikia kujirudia kwa ugonjwa huo hata pale wanapoamini hawana ugonjwa huo.

Ili kujua ukweli wa kinacholalamikiwa, Mwananchi limefanya uchunguzi katika vituo vya afya, hospitali za umma na binafsi na kubaini changamoto katika vipimo vya ugonjwa huo.

Gazeti linasimulia mbinu kadhaa za uchunguzi alizotumia mwandishi kupima vipimo mbalimbali katika zahanati na hospitali mbalimbali, ili kuthibitisha malalamiko ya Mwanahamisi.


Jaribio la kwanza

‘‘Saa 6:30 mchana natoka Mabibo jijini Dar es Salaam, kuelekea ilipo moja ya zahanati binafsi, umbali wa takriban nusu kilomita kutoka eneo nililokuwepo, nikiwa na maji kwenye chupa ndogo ndani ya begi nililobeba.

Nilipofika kwa daktari nilimweleza kwamba nahisi naumwa UTI, nikitaja dalili zote ninazohisi katika mwili, ikiwemo homa, maumivu wakati wa haja ndogo na kichwa.

Baada ya kuchukua maelezo yangu, daktari alinielekeza kwenda maabara kupimwa malaria na UTI. Nilichukuliwa damu kwa ajili ya kupimwa malaria, kisha nikapewa kichupa cha kuweka mkojo ili upimwe UTI.


Msalani niliingia na begi langu lenye maji niliyoyaandaa, hivyo badala ya mkojo kwenye kichupa nilichopewa na daktari wa maabara niliweka maji hayo, ingawa nilihofu pengine yangegunduliwa.

Ningefanyaje wakati nataka kujua ukweli kuhusu alichoniambia Mwanahamisi? Nilipeleka maji kama yalivyo, yalipokelewa na nikaelekezwa kwenda mapokezi kusubiri majibu ya vipimo.

Baada ya dakika 20 nilitakiwa kuingia katika chumba cha daktari kupokea majibu na maelekezo mengine ya kitabibu kama ulivyo utaratibu wa siku zote hospitalini.

Napata ugumu kueleza hofu niliyokuwa nayo, nikidhani pengine wamegundua kwamba nimepeleka maji na si mkojo. Hapo nikawa najipanga nitakavyojibu iwapo nitagundulika, lakini nikipanga kutumia mbinu hata ya kutimka mbio.


Mungu si Athumani kama wasemavyo wahenga, daktari alinijibu mkojo wangu (kiuhalisia ni maji tu ya kunywa) umekutwa na UTI, aliniandikia dawa na kunielekeza kupeleka taarifa katika dirisha la dawa.

Katika duka hilo nilipewa dawa zilizoandikwa Azuma-500 na nilielekezwa kumeza kidonge kimoja kila siku kwa siku tatu, kulingana na idadi ya tembe zilizokuwapo katika boksi hilo la dawa.

Baada ya mwezi nilirudi tena katika zahanati hiyo kufanya vipimo vile vile na awamu hii daktari alisema, nina maambukizi katika mirija ya mkojo hivyo napaswa kuchoma sindano tano.

Kabla ya kuchoma sindano moja niliyotakiwa kuanza wakati huo, niliomba kuelekezwa ilipo ATM kwa ajili ya kutoa fedha ya kugharamia dawa na nilitumia mwanya huo kutorudi tena kuepuka kudungwa sindano hizo.


Hapo nilijiridhisha kwa kiasi fulani kwamba majibu ya kukutwa na UTI kila unapokwenda zahanati kama alivyosema Mwanahamisi ni tatizo linaloweza kusababishwa na vipimo visivyo na uhalisia katika baadhi ya zahanati, hasa za binafsi.

Jaribio la pili

Katika kuthibitisha zaidi kauli ya Mwanahamisi, nilikwenda katika hospitali nyingine kubwa binafsi, iliyopo wilayani Ubungo.

Safari hii niliwaomba wanadada wawili wanisaidie kufanikisha uchunguzi wangu na tulianza safari kwa bodaboda mbili hadi ilipo hospitali hiyo.

Ilikuwa saa 2:18 usiku, ni mwendo wa dakika 10 kwa bodaboda tuliyokuwa tumepanda kutoka tulipokuwa hadi ilipo hospitali hiyo.

Tukiwa na maji mkononi kwa ajili ya kuyatumia katika uchunguzi huo, tulifika katika hospitali hiyo na kuingizwa katika chumba cha huduma za dharura.


Pamoja na huduma ya kwanza aliyopatiwa mgonjwa (mmoja wa mwanadada niliyekuwa naye) kulingana na maelezo yake, alitakiwa kupimwa UTI, wingi wa damu na sukari.

Wakati wa kupima UTI, alipewa kikopo kwa ajili ya kuweka mkojo na walipofika msalani na dada mwingine waliweka maji ndani yake kisha kurudisha maabara.

Ilichukua dakika 30 vipimo kukamilika, kisha daktari alimwita na kumpa majibu, niliomba kuwepo wakati wa majibu hayo.

Licha ya hospitali hiyo kutupa huduma nzuri ambayo inaweza kumpa faraja mgonjwa yeyote anayefika hapo, tatizo likawa kwenye majibu ya UTI.

Daktari alitujibu alichokuwa anakisoma kwenye kompyuta akisema; “damu yake ipo sawa, shinikizo la damu lipo sawa, hana malaria lakini ana UTI kali sana.”

Hatukupewa nakala ya majibu kwa wakati huo na baada ya kuiomba nilielekezwa kwenda maabara kutaja jina la mgonjwa, kisha nitapewa na baada ya kufuata utaratibu huo, nilifanikiwa kupata ripoti hiyo ya kimaabara.

Daktari alituandikia dawa aina ya Tinidazale, Norflox na Paradenk kwa ajili ya kwenda kuzilipia na kuzichukua katika duka la dawa la hospitali hiyo.

Badala ya kununua dawa nilipopata nakala (gazeti linazo) ya majibu ya vipimo niliyoandikiwa na daktari wa maabara, tuliondoka moja kwa moja hadi nyumbani.

Jaribio la tatu

Kama hiyo haitoshi, nilikwenda katika moja ya zahanati za umma kujiridhisha na vipimo, nikitumia maji ya bombani na hatimaye nayo yalikutwa na UTI.

Katika zahanati hii niliambiwa tatizo ni UTI na wingi wa damu na nilipewa dawa aina ya SPOTCLAV 625 na Meloxicam.

Jaribio la mwisho

Sikuishia hapo, katika kuthibitisha zaidi madai ya Mwanahamisi nilikwenda katika moja ya hospitali za rufaa jijini Dar es Salaam kuendelea na uchunguzi.

Hapa nilitumia maji ya bombani na tofauti na hospitali nilizoanza awali, hapo ilinichukua saa tatu kusubiri majibu ya vipimo na hata hivyo daktari alinijibu mkojo wangu haukuwa na shida.

Niliyoyakuta katika hospitali hiyo ndiyo yaliyotokea katika hospitali nyingine ya umma jijini humo, ambayo pia hakukuwa na changamoto ya vipimo, kwani sikukutwa na ugonjwa licha ya kutumia jaribio lile la kupima maji.

Si Mwanahamisi pekee

Kilichotokea kwa Mwanahamisi, pia kimetokea kwa Magreth Mondi na Abdallah Mpache wakazi wa Dar es Salaam, ambao nao wamelalamika kukutwa na ugonjwa huo mara kadhaa wanapokwenda hospitali.

“Yaani huchomoi hata ufanyeje lazima ukutwe na UTI. Zamani walikuwa wanasema si kila homa ni malaria, sasa hivi kila homa ni UTI,” anasema Magreth.

Ukweli kuhusu UTI

Licha ya majibu mazuri ya vipimo katika hospitali hizi, madaktari wa maabara walishindwa kugundua maji niliyopeleka badala ya mkojo, ambao kwa mujibu wa mtaalamu wa magonjwa ya binadamu, Profesa Andrea Pembe, vimiminika hivyo vina tofauti kubwa katika vipimo vya UTI.

Profesa Pembe anasema kuna tofauti kubwa ya mkojo na maji, hivyo wakati wa upimaji ni rahisi kugundua.

Akisisitiza hilo alisema: “Kwa sababu kinachopimwa ni specific gravity (tathmini ya ufanyaji kazi wa figo ili kutambua magonjwa ndani ya mkojo) ambayo kwa mkojo na maji ni tofauti kabisa.”

Katika kipimo cha UTI, anasema kinachoangaliwa ni kiwango cha wadudu ndani ya mkojo, chembe hai nyeupe za kupambana na magonjwa na naitrojeni inayozalishwa na wadudu kuwa ‘nitrates’ pamoja na seli zilizokufa za usaha, mambo ambayo hayapatikani katika maji.

Kuhusu maji kukutwa na UTI, Profesa Pembe kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), anasema UTI ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya mkojo pekee na si vinginevyo, hivyo maji hayawezi kuwa nao.

“Kwa sababu UTI ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya mkojo, maji ya kawaida hayawezi kuwa na UTI, haiwezekani kabisa na hata vimelea haviwezi kuwa huko,” alisisitiza.

Kauli ya mganga mkuu

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifello Sichwale, alisema uwezekano wa kipimo kutoa majibu kinyume na uhalisia, unasababisha na moja kati ya mambo matatu ambayo ni mashine husika, vitendanishi na weledi wa mtaalamu husika.

“Kwa upande wa mashine inaweza kufanya hivyo kama imetumika kwa muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo, maana matengenezo yanapaswa kufanywa kutokana na namna mashine inavyotumika,” alisema.

Alisisitiza kuwa jukumu la ubora wa mashine, vitendanishi na taaluma za wataalamu, linapaswa kufuatiliwa na waganga wakuu wa wilaya ama mkoa ilipo hospitali au kituo cha afya husika.

Kwa mujibu wa Dk Sichwale, katika kila robo ya mwaka, mganga wa wilaya au mkoa anatakiwa awe ametembelea vituo vilivyopo katika eneo lake walau mara moja.

“Hawa ndiyo wenye mamlaka ya kuhakikisha hospitali au vituo vya afya vilivyopo katika maeneo yao vinafanya kazi kwa kufuata miongozo ya Wizara ya Afya,” anasema Dk Sichwale. Alisema jukumu hilo hawapaswi kulitekeleza katika hospitali za umma pekee, bali hata binafsi wanatakiwa kufanya hivyo.

Hatari kunywa dawa za UTI

Kwa sababu wananchi hupewa tiba ya UTI ilhali hawaugui, Mfamasia mkuu wa Serikali, Daud Msasi anasema asili ya dawa yoyote ni sumu kwa ajili ya kuulia vimelea vya ugonjwa, hivyo ikitumika bila kuumwa inadhoofisha viungo vya mwili.

Alizitaja dawa hizo huchosha zaidi ini na figo, kwa kuwa zinapoingia mwilini zinapokelewa kama sumu na viungo hivyo huzipokea kwa ajili ya kuchuja hatimaye zigeuke mkojo.

“Figo na ini zinalazimishwa kufanya kazi ya ziada ambayo hazikupaswa kufanya kwa kutumia dawa kinyume na ugonjwa unaoumwa, hivyo madhara yake ni kufeli kwa figo na matatizo ya ini,” anasema.

Alishauri iwapo anayetumia dawa hizo bila kuumwa akafanikiwa kugundua, ni vema amalizie dozi ili kuepuka kuamsha vimelea vilivyopo mwilini kuanza kumshambulia na kisha visitibike kwa dawa yoyote kwa maana ya kutengeneza usugu.

Wataalamu maabara za afya

Wataalamu kutoka Chama cha Wataalamu wa Maabara za Afya ya Binadamu (MeLSATT), walisema kipimo cha UTI hutoka kati ya saa 48 hadi 72.

Kwa mujibu wa Roman Stephen, mwenyekiti wa dawati la habari wa MeLSATT, alisema siyo jukumu la wataalamu wa maabara kusoma matokeo ya vipimo, bali ni daktari.

“Daktari ndiye mtu atakayetoa tafsiri ya majibu ya vipimo kwa mgonjwa kulingana na mpangilio wa matibabu alioamua kuufuata kwa kuzingatia utaalamu wake,” alisema Stephen.

Alisema kuna wataalamu wasiozingatia kanuni za kutoa huduma ya afya, “mwenye ujuzi wa kusoma vipimo na haki ya kumueleza mgonjwa ni daktari,” alisema.

Kuhusu kipimo, Stephen alisema kwa kawaida wanapopokea mkojo wa mgonjwa maabara huuotesha kwa saa 24 hadi 48 ili kutazama kama una wadudu.

“Kufanya utambuzi wa mdudu na dawa inayoweza kumuua mdudu husika nayo inaweza kuchukua saa nyingine 24. Kwa hiyo jumla inaweza kuwa saa 72 au zikaongezeka.”

Hata hivyo, baadhi ya hospitali na zahanati zimekuwa zikitoa majibu ya vipimo hivyo ndani ya dakika 20 hadi 30 kama ambavyo uchunguzi wa gazeti hili umebaini katika maeneo iliyopita kupimwa.

Aidha, kumekuwa na udanganyifu kupitia ugonjwa wa UTI hivyo kuwatoza wagonjwa gharama za malipo ya kuona daktari, vipimo na dawa hasa kwa wagonjwa wa bi

NHIF yashtukia vipimo

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga alisema kumekuwa na udanganyifu mwingi ambao umekuwa ukifanywa na watoa huduma kuhusu vipimo, kikiwmao cha UTI, hali inayochangia kuumiza mfuko huo lakini wamekuwa wakipambana na hali hiyo.

“Udanganyifu upo na tumekuwa tukichukua hatua, tutasitisha mikataba ambayo itakuwa inahatarisha uendelevu wa mfuko. Kuna baadhi ya vituo ni rahisi kubambika dawa kwa mwanachama na tumekuwa tukiwabaini.

“Tumekuwa tukifuata mifumo kulingana na miongozo na tumekuwa tukichukua hatua ikiwemo kupiga faini, kuwaripoti wahusika katika mabaraza yao kama ni daktari basi tunatoa taarifa katika baraza la madaktari ili kuhakikisha tumelipia huduma halali kulingana na miongozo,” alisema.

Konga alisema ni kutokana na kuwapo kwa udanganyifu huo, walilazimika kuanza kufanya maboresho.

“Maboresho hayaepukiki na ni endelevu. Tumepokea maelekezo kutoka Wizara ya Afya na tumeyafanyia kazi maana ilileta taharuki,’’ alisema na kuongeza:

“Kwa mfano, maboresho tuliyoyafanya katika vipimo vya MRI na CT Scan kwamba lazima kuwe na kibali tulibaini wizi ulikuwa ukifanyika, vipimo ni Sh250,000 mpaka Sh400,000 walikuwa wanafanyiwa watu 800 kwa siku, lakini baada ya kuja na huo utaratibu wanapima 400 kwa siku, hivyo kulikuwa na udanganyifu.’’

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad