Waarabu wamuwekea Sakho milioni 800



 
KLABU ya wananchi ya Raja Athletic ya Morocco iko katika hesabu kali ikipigania saini ya winga wa Simba, Pape Sakho na fedha ambayo wameitaja kupata saini hiyo ni kama mtego kwa Wekundu wa Msimbazi.

Raja kupitia rais wao, Aziz El Badraoui wamepania kunasa saini ya winga huyo raia wa Senegal na tayari wameitengea Simba Dola 350,000 (takriban Sh815 milioni) ili wainase saini ya Sakho ambaye hivi karibuni alinyakua kiatu cha mfungaji wa bao bora la michuano inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kunyakua kiatu hicho, mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alikaririwa akisema tayari wanazo ofa kibao za wachezaji wao kutakiwa na timu mbalimbali Afrika akiwemo Sakho.

Inaelezwa Raja wameshafanya ushawishi kwa Sakho ambaye naye amewasukumia kwa mabosi wa klabu hiyo ili wamalizane, lakini mtego ni bado nyota huyo ana mkataba na Wekundu hao huku ofa hiyo ikiwa moja tu kati ya zingine nzuri ambazo Simba inazipima.


 
Badraoui ameliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu, wamevutiwa na Sakho na wako katika hatua nzuri ya kuwasilisha rasmi yao kwa wekundu hao baada ya kuongea kwa njia ya simu kupima kama wanaweza kumwachia mshindi huyo wa tuzo ya mfungaji wa bao bora la msimu la CAF.

“Tulianza kumfuatilia kwa muda mrefu Pape (Sakho) ni mchezaji mdogo mwenye kipaji, hapa Raja tunahitaji wachezaji wa kiwango kama hicho tutawasiliana kwa ukamilifu na Simba hivi karibuni, mchezaji hana tatizo,” alisema.

Wakati uongozi ukijipanga hivyo naye kocha wa timu hiyo mkongwe Faouzi Benzarti amekuwa akifuatilia taarifa zaidi za ubora za Sakho katika kujiridhisha zaidi.

Mwanaspoti linafahamu kwamba Faouzi ambaye ni kocha wa zamani wa Étoile du Sahel na Wydad Athletic amekuwa katika mawasiliano na makocha ambao wamewahi kukutana na Sakho akitaka kujua ubora wake zaidi.

Simba bado haijafanya uamuzi wa kipi ifanye katika ofa walizonazo juu ya Sakho huku pia Al Hilal ya Sudan ikipambana kunasa saini ya winga huyo.

Thamani ya Sakho imekuwa ikipanda zaidi hasa baada ya kushinda tuzo hiyo aliyokabidhiwa hivi karibuni nchini Morocco klabu nyingi zikifukuzana kusaka saini yake.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad