Watatu wafariki dunia, 36 wajeruhiwa ajali ya lori Handeni




Handeni. Wafanyabiashara watatu wamefariki dunia na wengine 36 wamejeruhiwa baada ya lori walilokuwa wamepanda wamepanda kwenda mnadani kuacha njia na kupinduka wilayani Handeni mkoani Tanga.

 Wafanyabiashara 11 hali zao zinasemekana sio nzuri kutokana na majeraha waliopata, hivyo wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya wilaya Handeni.

Akielezea tukio hilo mmoja wa majeruhi, Rajabu Juma amesema ajali hiyo imetokea asubuhi ya leo Jumapili Agosti 14 wakati wakielekea kwenye mnada kijiji cha Negero wilaya ya Kilindi.

, "Tulikuwa tunaelekea mnadani Negero tulifika eneo la Kwamagome wakati wa kukunja kona gari letu likaanguka" amesema majeruhi huyo


Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Handeni, Dk Hudi Shehdadi amekiri kupokea majeruhi 39 ambapo kati yao watatu walifariki dunia na kufanya kubaki majeruhi 36.

Amesema katika majeruhi hao 11 hali zao sio nzuri kutokana na majeraha waliyopata ila wanaendelea kupatiwa huduma na vipimo mbalimbali.

"Tulikuwa na majeruhi 39 waliopokelewa na kati yao watatu wamefariki dunia ambapo wawili ni wanaume na mwanamke mmoja lakini kwa maelezo ya madaktari 11 hali zao ni mbaya na wanaendelea na matibabu ili kuwanusuru", amesema Dk Hudi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji Handeni, Mussa Mkombati akiwa eneo la tukio amewasihi wafanyabiashara kuzingatia agizo la polisi la kutotumia malori kwenda mnadani, kwani mara nyingi usalama wake unakuwa mdogo.

"Serikali ilishatoa maelekezo kwamba wafanyabiashara wasitumie malori katika kusafiri kwenda mnadani, ila wamekuwa wakaidi na wanaendelea kupanda niliombe Jeshi la Polisi usalama barabarani kuendelea kuweka msisitizo wa kanuni hiyo", alisema Mkombti.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Sofia Jongo kuzungumzia ajali hiyo zimeshindikana ambapo msaidizi wake amepokea simu na kueleza kuwa kamanda yupo kwenye msafara wa kumpokea Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameanza ziara mkoani Tanga

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad